Katibu Mkuu Mbundi Aongoza Ujumbe wa Tanzania Kikao cha EAC Arusha

 



04 Septemba, 2025.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi ameongoza Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha maandalizi ya Mkutano wa 35 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango na Mkutano Maalum wa 58 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ngazi ya Makatibu Wakuu wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Mkutano huu wa ngazi ya Makatibu Wakuu umeanza jana tarehe 03 Septemba,2025, ambapo ni muendelezo wa vikao vya maandalizi ya Mkutano wa 35 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango na Mkutano Maalum wa 58 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, baada ya kuhitimisha vikao vya siku tatu ngazi ya Wataalam, vilivyoanza tarehe 31 Octoba, 2025 hadi tarehe 02 Septemba, 2025.

Kikao hiki kinahudhuriwa na Makatibu Wakuu kutoka nchi zote nane Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kenya, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Jamhuri ya Sudan Kusini, Jamhuri ya Uganda na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taarifa zilizopokelewa tangu ngazi ya Wataalam na zinazoendelea kujadiliwa katika ngazi hii ya Makatibu Wakuu ni pamoja na mapendekezo na taarifa mbalimbali za Jumuiya, ikiwemo Utekelezaji wa Maamuzi na Maelekezo yaliyopita ya Baraza la Kisekta la Mawaziri linaloshugnulikia masuala ya Afrika Mashariki na Mipango, Rasimu ya Mkakati wa Saba (7) wa Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2050, Mkakati wa Mageuzi ya Kidigitali wa Mwaka 2025 - 2030, Maandalizi ya Sera ya Lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Kalenda ya Majukumu ya Jumuiya kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2025 na hatua iliyofikiwa katika uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha Katika Jumuiya, na hatua iliyofikiwa katika masuala ya Kisiasa ya Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.

Kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu kinaongozwa na Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,  Bi. Caroline Karogo kutoka nchini Kenya kwasababu Kenya ndio Mwenyekiti wa Jumuiya kwa sasa.










Post a Comment

0 Comments