Mkinga, Tanga | Septemba 6, 2025
Mgombea Urais kupitia Chama cha NLD na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na ziara yake ya kampeni leo katika Wilaya ya Mkinga, ikiwa ni muendelezo wa kampeni za uchaguzi baada ya uzinduzi rasmi wa chama hicho.
Katika mikutano iliyofanyika katika vijiji vya Mtimbani na Moa, Mhe. Doyo aliwahutubia wananchi na kueleza kuwa wakazi wa ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi wamesahaulika na serikali iliyopo madarakani. Aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atawekeza kwenye sekta ya uvuvi kwa kununua meli kubwa zitakazosaidia wavuvi na vijana kupata ajira, pamoja na kujenga vituo vya usindikaji wa samaki ndani ya Wilaya ya Mkinga.
“Pamoja na hali ngumu mnayopitia, bado nyavu zenu mnachomewa badala ya kuwekewa mazingira mazuri ya uvuvi. Mkinipa ridhaa, nitahakikisha viwanda vya kusindika samaki vinajengwa katika ukanda huu ili vijana wapate ajira na kuuza bidhaa zao, ikiwemo samaki, kwa fedha za kigeni,” alisema Mhe. Doyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Ndugu Pogora Ibrahim Pogora, aliwataka wananchi wa Mkinga kutumia nafasi ya uchaguzi huu kuleta mabadiliko. Amesema kosa si kufanya mabadiliko, bali kuridhika na maisha magumu yanayoendelea kusababisha majuto.
“Tunawaomba wananchi msifanye makosa. Ili heshima yenu irudi, ni lazima kuleta mabadiliko kupitia kura zenu. Mpeni kura zote Mhe. Doyo ili aweze kushughulikia changamoto zenu,” alisema Pogora.
Kampeni za NLD zinaendelea kwa kasi, ambapo baada ya ziara ya Mkinga, msafara wa chama hicho unatarajiwa kuelekea Wilaya ya Muheza na kisha Korogwe.
0 Comments