Waziri wa Nishati January Makamba akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambao umefikia asilimia 86
Na Mwandishi wetu Rufiji
MRADI wa kufua Umeme wa Julius Nyerere umeanza kuonyesha faida baada ya kuzuia mafuriko katika baadhi ya mikoa ya Pwani na Morogoro.
Waziri wa Nishati January Makamba akiwa katika ziara ya kujionea ujazaji katika Bwawa leo Jumanne ,25 Aprili 2023 amewaambia waandishi wa habari kuwa ujazaji maji kwa kiasi kikubwa imezuia mafuriko yaliyokuwa yakiathiri wananchi.
“Tunafurahi kwamba tayari tumefikia mojawapo ya malengo makubwa ya kuanzishwa kwa mradi huu ambayo ilikuwa ni kuwakinga wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na mafuriko" alisema Mhe.Makamba.
Waziri Makamba ameleza kuwa kiasi cha mvua kilichoingia kwenye bwawa mwezi huu kinafanana na kile kilichonyesha miaka mitatu iliyopita na kuleta mafuriko katika mikoa ya Morogoro na Pwani.
“Kwa mvua hizi zilizonyesha katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na hasa siku mbili zilizopita, leo tungesikia taarifa za vifo na uharibifu wa mali, lakini kutokana na mradi huu, jambo hilo halijatokea mwaka huu,” alisema Waziri Makamba.
Akizungumza kuhusu mradi huo kwa ujumla, Waziri Makamba alisema kwa sasa mradi umetekelezwa kwa takribani asilimia 86 na kwamba kiwango cha maji kilichopo kinawapa matumaini juu ya lengo la mradi kuanza uzalishaji ifikapo mwezi Juni, mwaka 2024.
Akifafanua zaidi, Waziri Makamba alisema ili bwawa hilo lianze kuzalisha umeme kwa kiwango chake, linatakiwa kuwa na ujazo wa mita za ujazo bilioni 30 na sasa tayari kuna mita za ujazo bilioni 6 sawa na asilimia 20 ya kiasi kinachotakiwa.
Aidha, Waziri Makamba amewashukuru wataalamu na wafanyakazi wengine kwenye mradi huo kwa kufanya kazi kwa uzalendo na weledi na kuwataka wahakikishe wanamaliza kazi hiyo katika muda uliopangwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande, alimwahidi Waziri kwamba watahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kupunguza kero ya ukosefu wa umeme hapa nchini.
“Mwito wangu kwa wafanyakazi wenzangu wa TANESCO ni kwamba tusianze kuzembea kwa sababu tunaona kazi inakaribia kumalizika, huu ndio wakati wa kuchapa kazi bila kuchoka,” amesema Chande.
Desemba 22 mwaka 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi zoezi la kuanza kujaza maji katika mradi huo unaotarajiwa kuzalisha Megawati 2115 mara utakapokamilika.
Waziri wa Nishati January Makamba akikagua maendeleo ya ujenzi wa tuta kuu la kuzui maji ili kutengeneza bwawa.
0 Comments