DKT. MOLLEL ABAINISHA MIKAKATI YA KUPAMBANA DHIDI YA MAGONJWA YA SARATANI.

 


Na WAF, Bungeni, Dodoma. 

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kupambana dhidi ya magonjwa ya Saratani ikiwemo Saratani ya mlango wa kizazi. 

Amesema, Serikali ya Rais Samia imehakikisha hospitali zote za Rufaa za Mikoa zina CT-SCAN jambo linalosaidia huduma za ugunduzi wa mapema wa Saratani kushuka zaidi kwa wananchi katika ngazi ya mikoa.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Aprili 24, 2023 Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Taufiq Salim Turky Mbunge wa Mpendae, katika Mkutano wa kumi na moja.

"Serikali sasa hivi, kupitia Rais wetu Dkt  Samia Suluhu Hassan ametoa fedha na kuhakikisha hospitali zote za Mikoa zina CT-SCAN, maana yake hospitali zetu hizi za Mikoa zina uwezo wa kina wa kugundua mapema Saratani kabla hazijakua." Amesema Dkt. Mollel. 

Ameendelea kusema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya ipo kwenye mkakati mahususi wa kuwasomesha Wataalamu wa afya ili kuwapeleka katika hospitali za mikoa ili kushusha huduma hizo za Saratani.

Aidha, Dkt. Mollel amesema, Serikali imeendelea na mkakati wa Kampeni mbalimbali katika maeneo mbalimbali ikiwemo shule ili kuhakikisha elimu ya Saratani, ikiwemo elimu ya utoaji Chanjo ya mlango wa kizazi kwa wasichana wadogo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo. 

Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa Saratani kupitia vipindi vya redio na televisheni, machapisho na magazeti, mitandao ya jamii kama facebook, Instagram na pia televisheni za sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya.

Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amesema, Wizara itaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kuendelea kubaini sababu za saratani na namna bora ya kupambana dhidi ya ugonjwa huo nchini.

Post a Comment

0 Comments