Filamu ya Tanzania Royal Tour Yawakuna Wadau Seattle

 


Na mwandishi wetu Seattle, Washington State, Marekani


Wawakilishi wa taasisi mbalimbali za nchini Marekani hususani wa jiji lenye makao makuu ya taasisi nyingi za ubunifu na teknolojia la Seattle katika jimbo la Washington, wamefurahishwa na uzuri wa Tanzania mara baada ya kupata fursa ya kutazama sehemu ya filamu ya “Tanzania; The Royal Tour.”


Wawakilishi hao wakiongozwa na mmiliki wa klabu ya Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Marekani na mabingwa wa Mabara, Seattle Sounders, Adrian Hanauer, ambaye pia ni mwanahisa katika kampuni kubwa ya Amazon, walionekana wakishangilia na kupiga makofi katika sehemu mbalimbali za filamu hiyo huku wengi wakiahidi kuwa Julai mwaka huu watatembelea Tanzania.


“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi yetu kushika wadhifa huo, amejitoa kuwa kama mwongoza watalii na kuionesha nchi yetu katika filamu ya Royal Tour katika namna ambayo haijawahi kutokea. Karibuni sana Tanzania mje kujionea vivutio mbalimbali,” alisema Katibu Mkuu-Maliasili, Dkt. Hassan Abbasi, aliyeko katika ziara ya kikazi mjini humo akiambatana na Bw. Damasi Mfugale, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). 


Pamoja na Bw. Hanauer, mmiliki wa klabu ya Seattle Sounders, baadhi ya wawakilishi wa taasisi nyingine  kubwa na za kimkakati waliohudhuria hafla hiyo na kuitazama filamu ya Royal Tour ambayo pia ilioneshwa kupitia skrini kubwa za Uwanja wa Lumen (moja ya viwanja vitakavyotumika pia kwa fainali za Kombe la Dunia 2026) ni Bw. David Young, Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Klabu ya Seattle Seahawks, Andrea Bailey kutoka klabu ya NBA ya Portland Trail Blazers.


Wengine ni Michael Woody, kutoka kampeni ya Visit Seattle, Anbessie Yitbarek, Makamu wa Rais wa Masuala ya Biashara Ukanda wa Afrika kutoka kampuni ya Boeing, Reed Forrester Meneja Shirika la Ndege la Delta, AJ Jones II, Afisa

Mwandamizi wa Mawasiliano, kampuni ya Starbucks na Sarah Gavin, kutoka Makao Makuu ya Google.



Post a Comment

0 Comments