Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Mohamed Khamis Hamad jijini Dodoma leo Mei Mosi akitoa salamu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Mst. Mathew Mwaimu.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau mbalimbali kote ulimwenguni katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo husherehekewa tarehe Mosi Mei kila mwaka.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kwa mwaka wa 2023 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo:
“Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni Sasa.” Kauli mbiu hii inazungumzia umuhimu wa mishahara bora na ajira za staha kama sehemu muhimu ya ustawi wa wafanyakazi. Ibara ya 23 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua haki ya kila mtu kupata ujira wa haki kulingana na kiasi na sifa za kazi anazofanya.
THBUB inatambua na kupongeza juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuinua maslahi na kuweka mazingira bora ya wafanyakazi nchini.
Hivi karibuni, THBUB imeshuhudia kupandishwa mishahara, posho za kujikimu na kupandishwa vyeo kwa watumishi wa umma nchini.
Pamoja na jitihada hizo, THBUB imekuwa ikipokea na kushughulikia malalamiko kutoka kwa wafanyakazi yanayohusu maslahi yao kama vile kutopewa mkataba wa ajira, kutopandishwa madaraja, kutolipwa mishahara, kutopatiwa majibu ya rufaa zao na mamlaka za nidhamu, kupunjwa au kutolipwa posho mbalimbali ikiwemo posho ya kujikimu, posho ya likizo, posho ya kukaimu, posho ya kusafirisha mizigo, n.k.
Pia, THBUB imekuwa ikipokea na kufuatilia madai ya wafanyakazi yanayohusu michango yao ya kila mwezi kutowasilishwa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kutopatiwa matibabu chini ya Mfuko wa Bima ya Afya, madai ya fidia ya kuumia kazini, kutolipwa au kupunjwa mafao baada ya kustaafu kazi na malipo ya pensheni ya kila mwezi.
Kupitia siku hii, THBUB inawakumbusha Waajiri kuhusu umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya kazi kwa wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, kuwashirikisha wafanyakazi katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia mipango ya taasisi, kuepuka ubaguzi na matumizi ya lugha chafu na udhalilishaji wa kijinsia.
Serikali na waajiri waendelee kusimamia utekelezaji wa Katiba, sheria za ajira na kuweka mazingira bora ya kazi ili kuhakikisha ajira zinazingatia heshima na utu wa mtu.
Katika kuhakikisha usimamizi wa viwango vya ajira nchini, ni muhimu pia Serikali kupitia taasisi zinazohusika chini ya Wizara zinazohusika na Kazi, Ajira na Utumishi wa Umma Tanzania Bara na Zanzibar kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara, hususan katika sekta binafsi ili kuhakikisha haki za wafanyakazi kama zilivyobainishwa katika sheria zinazohusiana na masuala ya ajira zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara kwa wakati na yenye kuzingatia kiwango cha chini cha mishahara, usalama na afya mahali pa kazi, matibabu, malipo ya fidia inayotokana na kuumia kazini na michango ya hifadhi ya jamii.
Kwa kuzingatia kuwa haki inaendana na wajibu, THBUB inawakumbusha wafanyakazi wote kutekeleza majukumu yao kwa juhudi na maarifa na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia ajira zao.
Aidha, wafanyakazi wajielekeze katika kuzingatia maadili na kutoa huduma zenye viwango kwa uadilifu.
THBUB inaamini kuwa waajiri na wafanyakazi wakitekeleza wajibu wao ipasavyo, Mishahara Bora na Ajira za Staha kwa Maendeleo ya Wafanyakazi zitapatikana.
0 Comments