Na mwandishi wetu
SHIRIKISHO la Vyama vya wafanyakazi (TUCTA) limempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mishahara.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA Saidi Wamba akizungumza na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya Sherehe za Mei Mosi Mwaka huu.
Amesema kwamba wamekuwa na mafanikio makubwa katika Sherehe hizi hususan Awamu hii ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Awamu ya Tano hatukuwahi kupata hata nyongeza ya mishahara, lakini Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia, amefanya nyongeza ya mishahara,” amesema Wamba.
Wamba amesema pamoja na changamoto ya nyongeza hiyo kutofikia wafanyakazi wote wanaamini hilo linaweza kushughulikiwa kwa mazungumzo.
Hata hivyo ameipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuongeza nyongeza hiyo kwani imejaribu kushughulikia maombi yao.
Kwamba wataendelea kuishauri Serikali kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Amesema sio rahisi kwa Serikali kutatua changamoto zao mara moja kwani zimelundikana kwa takribani miaka Sita bila kushughulikiwa.
“Kinachotutia moyo ni kwamba Serikali imefungua milango ya majadiliano na wafanyakazi,” ameongeza Wamba.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa tija, kwamba wanapodai maslahi basi na wao watimize wajibu wao.
0 Comments