WANAWAKE VIJANA JISHUGHULISHENI NA BIASHARA PAMOJA NA UJASIRIAMALI - KAPINGA

 


Na mwandishi wetu


Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, amewataka Wanawake Vijana kujishughulisha na Biashara pamoja na Ujasiriamali ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi.

Wito huo umetolewa tarehe 11 Novemba 2023 wakati alipofanya ufunguzi wa Kongamano la Taasisi isiyo ya Kiserikali ya
Ladies Talk Tanzania Initiative inayojishughulisha na masuala mbali mbali ya kijamii pamoja na Ujasiriamali lililofanyika mkoani Morogoro.

"Niseme ukweli ya kwamba, ni nia ya dhati kabisa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutaka Wanawake wote nchini na duniani kote kusonga mbele kiuchumi, kuwa walezi wazuri wa familia na viongozi katika Sekta mbalimbali katika ngazi mbalimbali za uongozi,"Amesema Naibu Waziri Kapinga.

Naibu Waziri Kapinga amewasisitiza Wanawake Vijana kujishughulisha na Ujasiriamali na kushikana mkono pale wanapofanikiwa kufikia hatua fulani ya maendeleo katika biashara na shughuli za Ujasiriamali.

"Naamini kabisa, kwa kila mmoja wenu hapa, hatua uliyofikia, kuna mtu alikushika mkono. Hivyo ni muhimu sana kukumbuka, unapoinuka juu kiuchumi, kumbuka kuwashika mkono wengine ambao wanahitaji kutiwa moyo, kuhamasishwa na kuwezeshwa kupiga hatua katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara na ujasiriamali kama shughuli hizi mnazozifanya." ameeleza kwa hisia Naibu Waziri Kapinga.

Aidha, Naibu Waziri Kapinga amewataka wanawake vijana kutohofia kuanza kujishughulisha na wazo jipya la kibiashara au ujasiriamali kwa kuhofia kutofanikiwa katika shughuli husika.

" Kijana usiishi ndoto za watu wengine, kile ambacho unafanya ndicho hicho ukisimamie na ufanye kwa bidii na kukipenda. Uanze sasa kwa chochote ulicho nacho haijalishi ni kikubwa au kidogo". Amesema Mhe. Kapinga.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Kapinga amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa *Ladies Talk Tanzania* Bi. Salome Sengo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusaidia jamii na kutoa elimu ya Ujasiliamali kwa Wanawake Vijana.

Kwa upande wake Mtendajii Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) Dkt. Sophia Kashenge amewasisitiza Vijana kuwa na uthubutu katika kujiajiri na kuona ni vitu gani wanaweza kufanya ili kujikwamua kiuchumi, na kufikiria kitofauti kufanya kilimo chenye tija.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ladies Talk Tanzania Initiative Salome Sengo amemshukuru Naibu Waziri Kapinga kwa kuhudhuria Hafla hiyo pamoja na kutambua ushiriki na uwepo wa wadau mbali mbali wa Ujasiriamali waliowezesha, kufanikisha kongamano hilo.

Kongamano hilo la siku moja limeshirikisha Wanawake Vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments