Dkt. Diallo aeleza sababu matumizi hafifu ya mbolea Kanda ya Ziwa

 



Na mwandishi wetu


Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo ameeleza kuwa, uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya mbolea unawafanya wananchi wa Kanda ya Ziwa kutokutumia mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.

Ameeleza sababu nyingine kuwa  ni kutokuzingatia suala la upimaji wa afya ya udongo unaopelekea kutokuwa na taarifa sahihi ya virutubisho vinavyohitajika kwenye udongo wanaoulima.

Dkt. Diallo amezungumza hayo tarehe 15 Aprili, 2024 katika kikao kifupi na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda alipofika ofisini kwake kueleza lengo la ziara ya bodi na menejimenti ya TFRA mkoani Mwanza.

"Nafahamu usipotumia mbolea mfano kilimo cha pamba kwenye ekari moja wanapata Kilo 220- kilo 230 kwa ekari ambayo ni sawa na kupoteza muda kwani wangeweza kupata kilo 800 hadi 1000 endapo wangetumia mbolea" Dkt. Diallo alisisitiza.

Amewataka wakulima kuwatumia maafisa ugani wa maeneo yao kupima afya ya udongo na kuwapa ushauri wa kitaalamu juu ya aina ya mbolea wanayotakiwa kutumia kulingana na majibu ya vipimo. 

Aidha, amewataka viongozi wa mkoa huo kusimamia suala la usahihi wa takwimu zinazotolewa na maafisa ugani ili kuisaidia Wizara ya Kilimo katika kupanga na kuweka sawa malengo na mikakati ya kutekeleza kwa vipindi vinavyofuata.

Naye, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Daniel Machunda ameeleza kukubaliana na Dkt. Diallo na kueleza wananchi wake bado hawajapata uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya mbolea na kukiri maafisa kilimo wa mkoa na wilaya zake wanakazi kubwa ya kutoa elimu na kusaidia kubadilisha mtazamo wa wakulima wao.

Ameahidi ofisi yake kuendelea kuwahimiza wakulima kutumia mbolea pamoja na  kusimamia maelekezo ya kitaifa ya kuhakikisha wakulima wanasajiliwa kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku.





Post a Comment

0 Comments