HOSPITALI YA MUHIMBILI YAZINDUA MASHINE YA KISASA YA KUCHUNGUZA SARATANI.

 


Na mwandishi wetu


HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imezindua mashine mpya ya kisasa (Senographe Pristine 3D Mammography suite) Yenye uwezo mkubwa wa kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti kwa njia ya kisasa zaidi.



Mashine hiyo imezinduliwa kwa kushirikiana na GE Healthcare na Chama cha Mionzi cha Amerika Kaskazini (RSNA).



Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo leo Aprili 17,2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea amesema ufungaji wa mashine hiyo ni jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya afya.



"Kulingana na takwimu za Shirika la kimataifa la Afya (WHO), wanawake milioni 2.3 wamegunduliwa na saratani ya matiti. Ila kwa Tanzania, wanawake 42,000 wanagundulika kuwa na saratani ya matiti lakini cha kusikitisha ni kwamba asilimia 38 pekee ndio wanaopata matibabu, ikimaanisha kuwa ni wanawake 15,000 pekee wanaopata matibabu,” amesema Dkt. Nyembea .



Akiishukuru serikali ya Marekani na RSNA ameeleza kuwa mahusiano baina ya nchi hizo yamekuwa muhimu katika upatikanaji wa teknolojia ya hali ya juu inayohitajika ili kuongeza uchunguzi na utambuzi wa saratani ya matiti kwa wanawake nchini.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MNH, Prof.Mohammed Janabi amesema kuwa mashine hiyo mpya itawezesha utambuzi wa mapema na kuokoa maisha ya wanawake wengi nchini huku akibainisha kuwa saratani ya matiti ndiyo saratani inayowapata wanawake wengi na kwamba wanaongezeka.



“Muhimbili ni mwanga wa matumaini. Tunatarajia kwamba angalau wagonjwa 200 kwa mwaka hadi 2,400 watafaidika moja kwa moja kutokana na uchunguzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Ninaahidi kwamba mashine yetu ya uchunguzi wa saratani ya matiti (Senographe Pristina 3D) itahudumia watu wote kwa weledi wa hali ya juu na utunzaji bora,” amesema.



Amesema kuwa, mashine hiyo inatumia kiwango kidogo zaidi cha mionzi na hivyo kuifanya kuwa salama zaidi kwa watumiaji.



Aidha ametaja sifa za mashine hiyo kuwa itasaidia katika huduma za kiuchunguzi za matiti za kawaida (Core mammography functions), huduma za kiuchunguzi za kibobezi za matiti ambapo mgonjwa atachomwa sindano ya dawa ambayo wakati wa kupiga picha dawa hiyo hujikusanya zaidi kwenye maeneo yanayohisiwa kuwa na shida mathalani kwenye saratani kuonekana vizuri zaidi kwa waataalamu.



Amesema kuwa mashine hiyo ina uwezo mkubwa wa kuwaongoza wataalamu kutambua tatizo kwa usahihi wa hali ya juu na pia kutoa kinyama (sample) kwenye matiti kwa ajili ya uchunguzi pindi itakapohitajika



Kumekuwepo na uelewa mdogo katika jamii kuhusu saratani ya matiti, watu hawajui kuwa huduma za matibabu zinapatikana kwa urahisi kuanzia ngazi ya vijijini hadi ngazi ya taifa. Napenda kuwaambia wananchi kuwa huduma hizi zipo na zimeboreshwa vizuri. Ni wakati muafaka kwa wananchi kwenda kwenye vituo vya afya vilivyo karibu ili kupima afya zao na kupata ushauri wa kiafya.” ameongeza Prof. Janabi



Naye, Eyong Ebai, Meneja Mkuu wa Kanda ya Afrika mwa Jangwa la Sahara katika GE Healthcare, amesema wanasherehekea usimikaji wa hospitali ya kwanza ya umma nchini Tanzania na kuwa mwenyeji wa mfumo kamili wa mammografia wa digitali iunaotarajiwa kutoa huduma bora .



"Ni muhimu kutambua kuwa saratani ya matiti katika vidonda vinavyotiliwa shaka. Mifumo hii itawezesha utambuzi wa haraka wa saratani ya matiti ambayo itaokoa maisha".



Amesema kuwa wataendeleza mapambono hayo kwa kuwajengea watu uwezo ambao wataongoza kliniki kote Tanzania na ukanda mzima katika mapambano dhidi ya saratani ya matiti,.



“Tutapima na kutathmini viashiria vinavyoongoza ili kufuatilia maendeleo na kuhakikisha tunafanikiwa. Tutatayarisha na kutoa programu za elimu ili kujenga uwezo ili kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu. Tutatoa data na taarifa muhimu ambazo zitaendesha sera, udhibiti na ugawaji wa rasilimali kwa msingi wa ushahidi ili kuboresha matibabu ya saratani ya matiti nchini Tanzania." amesema 



Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa wa Chama cha Mionzi cha Amerika Kaskazini (RSNA) Meredith McNeil alisema pamoja na ufungaji wa mashine ya Pristina Mammography nchini Tanzania, teknolojia hiyo itasaidia kuhakikisha wanawake wanapata uelewa wa saratani ya matiti, matibabu, uchunguzi wa jumla na kinga na kuongeza kuwa. , bado kuna safari ndefu ya kupata watu wengi mafunzo na kuwavutia wanawake. "Kwa kweli hii itakuwa mfano kutoka Tanzania hadi ukanda wa Afrika juu ya kile ambacho mammografia inaweza kutoa kwa idadi ya watu, ikizingatiwa kuwa huduma ya afya ya wanawake huathiri sana familia kwa hivyo tunatarajia kuwa mfano huu unaweza kusaidia sana katika utunzaji wa kawaida na kusaidia kuokoa pesa." Amesema.

Post a Comment

0 Comments