Na mwandishi wetu
*Imeshika nafasi ya Kumi kwa uzalishaji wa Kinywe Duniani*
*Unamilikiwa na Mtanzania kwa asilimia 100*
Mradi wa Uchimbaji na Uchenjuaji Madini ya Kinywe wa GODMWANGA JEMS LIMITED uliopo katika eneo la Kwamsisi, wilaya ya Handeni Mkoani Tanga unatajwa kuwa mradi wa kwanza Barani Afrika kwa uchimbaji na uchenjuaji wa Madini hayo na hivyo kushika nafasi ya kumi Duniani.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Mradi wa *GODMWANGA-B* Henri Joseph wakati akizungumza na timu ya Maafisa Habari kutoka Wizara ya Madini na Wataalamu wa Tume ya Madini.
Akizungumza na timu hiyo, Joseph amesema mradi huo umekuwa ukifanya vizuri katika uzalishaji wa madini hayo na unatarajiwa kuzalisha tani 800 kwa siku baada ya ujenzi wa kiwanda kipya kukamilika ifikapo Oktoba 2024.
Aidha, Joseph amesema mradi huo umejikita zaidi kwenye uzalishaji wa Madini Mkakati ambapo kwa sasa Dunia inauhitaji mkubwa wa madini hayo yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme, betry za simu, oil, grisi, penseli na vizuia joto.
Pia, Joseph ameeleza kuwa, Mgodi huo umefanikiwa kuigusa jamii kwa kuchangia huduma ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa cha Afya chenye thamani ya shilingi Milioni 200, kujenga Madarasa 6 ya shule ya Sekondari Kitumbi, kukarabati jengo la Mahakama na kukarabati barabara ya kuelekea shule ya Sekondari Kwamsisi iliyopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa *GODMWANGA-A* James Minja amesema Kampuni hiyo imefanikiwa kuajiri zaidi ya Wafanyakazi 200 wa kudumu na wafanyakazi 300 wa mkataba kwa lengo la kuinua vijana kiuchumi na kuendeleza uzalishaji wa Madini hayo kwa wingi.
Minja amesema kwa muda mfupi tangu kuanzishwa kwa mradi huo wamefanikiwa kupata soko kubwa la madini hayo katika nchi mbalimbali ikiwemo China na India.
Ameongeza kuwa, mpaka kufikia Oktoba mwaka 2024 kampuni hiyo itakuwa imekamilisha ujenzi unaoendelea wa mradi mkubwa zaidi ya mara kumi ya ulipo sasa ambapo inatarajiwa kuongeza uzalishaji na kupelekea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi Tano Duniani zinazo zalisha madini ya Kinywe kwa kiwango kikubwa.
Pamoja na mambo mengine, Minja ameishukuru Serikali na kuomba kusaidiwa kuboreshewa miundombinu pamoja na huduma zingine hususan huduma za upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika.
0 Comments