TAWA YAFANYA MSAKO WA MAMBA TISHIO KWA MAISHA YA BINADAMU RUFIJI

 



Na mwandishi wetu


Katika kuhakikisha usalama wa maisha ya watu  wilayani Rufiji, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imefanya msako wa mamba  wanaotajwa kutishia maisha ya watu kutokana na kusogea karibu na makazi ya watu kufuatia kusafirishwa na mikondo ya maji yaliyosababishwa na mafuriko.


Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja akizungumza na waandishi wa habari katika mji mdogo wa utete wilayani Rufiji leo Aprili 18, 2024 amesema TAWA inaendelea na msako wa mamba tishio kwa maisha ya watu wilayani humo lengo likiwa ni kulinda  usalama wa wananchi wa wilaya hiyo. 


" Ni wajibu wetu kuimarisha ulinzi ili yasitokee maafa ya binadamu kupotea kutokana na  kuliwa na mamba wakati  sisi tuko hapa" amesema Afisa habari huyo.


"Na ndiyo maana tumekuja hapa kuhakikisha tunawasaka mamba wote ambao ni tishio kwa maisha ya binadamu.


Aidha Maganja amesisitiza kuwa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Sura ya Na. 283 inaelekeza kuwadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu endapo itaonekana wana hatarisha maisha ya binadamu, hivyo chochote wanachokifanya ni kwa mujibu wa sheria lengo likiwa ni kulinda uhai wa binadamu.


Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuzingatia elimu wanayoendelea kupewa na Maofisa uelimishaji kutoka TAWA ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwa kushambuliwa na mamba.


Naye Afisa Mhifadhi wa TAWA George Boniface amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mamba wengi wamesafirishwa na maji kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere na Hifadhi ya Selous na kufika katika  maeneo ya makazi ya watu katika mji wa utete na viunga vyake wilayani Rufiji kiasi cha kutishia maisha ya binadamu.


Amesema zoezi linaloendelea eneo hilo ni kuwasaka mamba wote ambao ni tishio kwa kutega mitego na kwa kutumia boti kwa usaidizi wa wenyeji na wavuvi.


Vilevile, Hamis Moshi Ipombo ambaye ni mzaliwa na mkazi wa utete Rufiji anayejihusisha na shughuli za uvuvi amesema katika mto Lugongwe uliopo eneo la utete kumekuwepo na mamba  mkali anayetishia maisha wakazi wa eneo hilo kwa kukimbiza mitumbwi wawapo katika shughuli zao, mamba anayetajwa kusakwa na Maofisa wa TAWA.


 Hata hivyo ameishukuru Serikali kupitia TAWA kwa kuwapata elimu ya kuepuka madhara yatokanayo na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba huku akikiri kuwa elimu hiyo imewasaidia kuendelea na shughuli zao za kiuchumi huku wakiwa salama.







Post a Comment

0 Comments