Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo (kulia) akizungumza na wafanyabiashara wa mbolea wa Mkoa wa Mwanza tarehe 15 Aprili,2024 katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa mikutano mkoani hapo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Robert Mtendamema akizungumza na wafanyabiashara wa mbolea (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi mdogo wa mikutano ndani ya ofisi za mkuu wa wa Mkoa wa Mwanza tarehe 15 Aprili, 2024.
Na mwandishi wetu
Wafanyabiashara wa mbolea mkoani Mwanza wametakiwa kushirikiana na serikali katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili kuwasaidia kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao wanayoyalima.
Wito huo umetolewa leo tarehe 15 Aprili, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo wakati wa kikao na wafanyabiashara wa mbolea wa Mkoa huo.
Dkt. Diallo amesema, tokea Serikali ianze kutoa ruzuku kwenye mbolea kumekuwa na ongezeko la mavuno kutoka tani Milioni 7 hadi kufikia tani Milioni 12 jambo linaloonesha tija itokanayo na matumizi ya mbolea kwenye shughuli za kilimo.
Amesema, Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa isiyotumia mbolea kutokana na imani potofu kuwa mbolea inaharibu udongo suala ambalo si kweli.
Ameongeza kuwa, matokeo hafifu ya uzalishaji hayatokqnani na matumizi ya mbolea za viwandani isipokuwa husababishwa na wakulima kutumia mbolea bila kupima na kufahamu mahitaji halisi ya udongo na hivyo kutumia mbolea sahihi.
"Sasa tunachoomba kwenu wafanyabiashara, jaribuni kuwa waalimu, mbolea mnazouza mnajua ubora wake na mnajua zinahitaji kutumika kwenye aina gani ya udongo, waelimisheni wateja wenu". Dkt. Diallo alisisitiza
"Msipende kuuza mbolea kwa wakulima bila kujua aina ya udongo anaokwenda kutumia maana zisipompa majibu mazuri hatorudi tena kununua mbolea kwako na utakuwa umempoteza" Dkt. Diallo alisisitiza.
"Jukumu letu ni la udhibiti, hivyo tunajikita katika kuangalia ubora wa mbolea zinazouzwa na uzingatiaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa mkulima" Dkt. Diallo aliongeza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TFRA, Robert Mtendamema amesema, lengo la ziara mkoani humo ni kuhakikisha biashara ya mbolea inafanyika kwa kufuata sheria ya mbolea na wakulima wanapata mbolea bora kwa wakati ili kupelekea tija na kuinua uchumi wao.
Amewataka wafanyabiashara kuwahamasisha wakulima kujisajili na kujikita katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kupitia mashamba darasa ili wakulima wajifunze kwa kuona na kuwasaidia kuongeza matumizi ya mbolea na kuongeza tija kwenye shughuli zao za kilimo.
Wafanyabiashara wa mbolea wa Mkoa wa Mwanza wakifuatilia maelekezo ya Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo
Watumishi wa TFRA na Wafanyabiashara wa mbolea wa Mkoa wa Mwanza wakisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo wakati wa kikao baina ya Wajumbe wa Bodi, Menejimenti ya TFRA na wafanyabiashara hao katika ukumbi mdogo wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 15 Aprili, 2024.
Wafanyabiashara wa mbolea wa Mkoa wa Mwanza wakifuatilia maelekezo ya Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo tarehe 15 Aprili, 2024.
Mfanyabiashara wa mbolea mkoani Mwanza akichangia mada wakati wa kikao baina yao na wajumbe wa bodi na Menejimenti ya TFRA tarehe 15 Aprili, 2024
0 Comments