*OFISI YA MBUNGE JIMBO LA MOROGORO MJINI*
*MHE, ABOOD* AFAFANUA UMUHIMU WA UZINDUZI WA TRENI YA KISASA YA MWENDOKASI NA KUINUA UCHUMI WA MKOA MOROGORO.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini *Mhe, Abdulaaziz M. Abood* ameeleza umuhimu wa uzinduzi wa Treni ya Mwendokasi Mkoani Morogoro, uzinduzi ambao umeanzia Mkoani Dar es Salaam, Morogoro na kuishia Mkoani Dodoma, ambapo kimsingi unaleta matumaini mapya katika shuluhisho la kudumu la usafiri na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia biashara na Taifa kwa ujumla.
*Mhe Abood* ameeleza umuhimu huo Agosti Mosi mwaka huu wa 2024 wakati akizungumza mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan* kwenye Kituo Kikuu cha Treni hiyo Mkoani Morogoro kilichopo Kihonda kwa Chambo, ambapo amesema, kukamilika kwa Reli hiyo ya Kisasa kutalinufaisha Jimbo la Morogoro Mjini kwa kiasi kikubwa kupitia Nyanja mbalimbali za kiuchumi.
Aidha, *Mhe Abood* ameweka wazi kuwa, umuhimu wa Mradi huo wa Reli ya Kisasa kwa Mkoa na Jimbo la Morogoro Mjini ni mkubwa sana ukizingatia, Morogoro ni Mkoa wenye vivutio vingi vya Utalii hivyo utaweza kuunufaisha kwa kuongezeka Watalii na wawekezaji hali itakayopelekea wananchi na Wajasirimali, wafanya kazi za usafirishaji wenye Mahoteli Makubwa kutumia vyema fursa hizo na hatimaye kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa.
*“Treni hii inaongeza uchumi katika Manispaa yetu, inaongeza uchumi katika Mkoa wetu wa Morogoro kwa Uwekezaji kwani jambo hili la leo ni muhimu kwako wewe Mhe. Rais pamoja na sisi wana Morogoro.” Ameweka wazi Mhe Abood.*
Vilevile, *Mhe Abood* ametoa shukrani za dhati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuwa *Mhe, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan* amefanikisha miradi mingi katika Manispaa ya Morogoro inayolenga kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa huduma za kijamii katika Sekta za Maji, Umeme, Nishati, Miundombinu, Afya na Elimu.
Zaidi, *Mh Abood* amewataka watanzania wote kwa nguvu Moja bila kujali tofauti za Kichama kumuunga mkono *Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania* ikiwemo kumuombea na kumpa Moyo ili aendelee kulitumikia vema kwa kuliteletea maendeleo taifa la Tanzania, kwani hayo ndio yatakuwa malipo stahiki.
Imetolewa na; *Idara ya Habari na Mawasiliano Ofisi ya Mbunge*
0 Comments