Na mwandishi wetu
Ikiwa ni siku ya tatu katika kuadhimisha sikukuu za wakulima zilizoambatana na maonesho yanayofanyika kanda zote nchini na Dodoma yakiwa yanafanyika kimataifa, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania imeendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na tasnia hiyo.
Akijibu swali lililoulizwa na watembeaji kutoka mradi wa Kilimo Tija Kigoma chini ya World Food Programme (WFP) kwenye banda waliotaka kujua endapo Mamlaka inadhibiti na kusambaza mbolea kwa wakulima, Mwahija Irika, Meneja Usajili na leseni TFRA, amesema Mamlaka inadhibiti ubora na biashara ya mbolea na haisambazi mbolea moja kwa moja kwa wakulima.
Ameongeza kuwa, Mamlaka ina jukumu la kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati kwa njia ya kutoa vibali vya uzalishaji na uingizaji wa mbolea nchini, na kusajili wafanyabiashara wa mbolea walioko katika ngazi ya halmashairi, kata na vijiji ili kuwa na uhakika kuwa mbolea inamfikia mkulima karibu na eneo lake.
Akijibu hoja kuhusu uwepo wa mbolea zinazoharibu udongo na namna wanavyoweza kuzitambua Steven Gossy Afisa Udhibiti Ubora wa TFRA ameeleza kuwa, Mbolea zote zilizosjiliwa na TFRA zikitumiwa ipasavyo, kwa maana ya kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea haziharibu udongo na kubainisha kuwa mbolea inaharibu udongo pale inapotumika ndivyo sivyo.
Ili kuwawezesha kuwa na uelewa mkubwa amewapa mfano na kueleza namna Wizara ya Kilimo ilivyojipanga kuwawezesha waulima kulima kwa tija kwa kuwezesha vifaa kwa ajili ya kupima afya ya udongo wa mkulima na kupitia maafisa ugani aweze kushauriwa aina sahihi ya mbolea inayofaa kulingana na mahitaji ya udongo husika.
Amewaasa wakulima kuwatumia maafisa ugani waliopo katika maeneo yao ili waweze kupewa ushauri wa kitaalam katika kuendesha shughuli zao za kilimo ikiwemo uandaaji wa mashamba, uchaguzi wa mbegu pamoja na ushauri kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.
Katika hatua nyingine Mamlaka imeendelea kutoa elimu kwa vitendo kwenye vipando vya zao la alizeti ndani ya viwanja vya nanenane Nzuguni Jijini Dodoma ambapo Meneja wa sehemu ya Udhibiti Ubora na Majaribio, Scholar Mbalila alieleza tofauti iliyopo baina ya shamba lililopandwa bila mbolea, lililopandiwa mbolea aina ya samadi, lililopandiwa mbolea za viwandani na zile zilizopandiwa mbolea za mchanganyiko wa mbolea za samadina za viwandani ambapo mbolea zenyemchanganyiko zimeonesha kufanyavizuri zaidi kwenye ukuaji wa mmea.
Akieleza sababu za mimea hiyo kuonesha ukuaji unaoridhisha, Mbalila amesema ni kwa sababu imepata virutubisho vyote 14 vinavyohitajika na mmea.
Amesema, Mamlaka iliamua kutoa elimu kupitia zao la alizeti kutokana na utafiti kuonesha kuwa asilimia 80 ya wakulima wa zao hilo kutokutumia mbolea na hivyo kuwa na mavuno duni tofauti na ambavyo wangevuna mara baada ya kutumia mbolea.
Akitoa neno la shukrani mmoja wa wanajumuia wa mradi wa Kilimo Tija Kigoma, Apolinary Kitwe alisema jukumu lao muhimu ni kuhakikishawakulimawanatumia pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea hivyo kufika bandani hapokumewawezesha kupata majibu ya maswali yao ikiwa ni pamoja ya namna wakulima wanaweza kupata mbolea kwa urahisi na kwa wakati pamoja na kutatuliwa changamoto ya kupata namba za kununulia mbolea.
TFRA imeendelea na maonesho katika maeneo mbalimbali ambapo kwa Mkoa wa Morogoro katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere Banda la Mamlaka limetembelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri aliyekuwa mgeni rasmi wa maonesho wa siku katika viwanja hivyo.
0 Comments