WANACCM WASISITIZWA KUSHIKAMA KUJENGA OFISI ZA KATA WILAYANI GEITA

 




Na mwandishi wetu

Katika jitihada za kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kimezindua rasmi ujenzi wa ofisi za chama hicho katika Tawi la Mwatulole, Kata ya Buhalahala, Wilayani Geita. Rais Samia alitoa agizo la kila kata nchini kuwa na ofisi za chama ili kusimamia vyema shughuli za maendeleo ya chama na wananchi.

Akizindua ujenzi huo, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Geita, Gabriel Nyasilu, alisisitiza ushirikiano wa wanachama ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati. Aliwaomba wanachama kushirikiana kwa hali na mali ili ofisi hizo ziweze kuanza kutumika ifikapo Desemba mwaka huu.

Katika uzinduzi huo, Nyasilu aliendesha harambee na kufanikiwa kukusanya jumla ya mifuko ya simenti 250, matofali 4500, pamoja na fedha taslimu shilingi elfu 50. Hii ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Nyasilu pia alimwagiza Mwenyekiti wa Tawi la Mwatulole kuhakikisha ujenzi wa ofisi hiyo unakamilika kabla ya Desemba mwaka huu, ili ifikapo mwisho wa mwaka jengo hilo lianze kutumika rasmi.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Buhalahala, Mussa Kabesa, alisema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 90. Aliongeza kuwa ujenzi utaanza mara moja ili kuhakikisha lengo la kukamilisha ifikapo Desemba mwaka huu linafikiwa.

Ujenzi huu ni sehemu ya juhudi za CCM kuhakikisha kata zote nchini zinakuwa na ofisi za kisasa kwa ajili ya kusimamia na kuratibu shughuli za chama kwa ufanisi na kuwa karibu zaidi na wananchi.

Wanachama wa CCM Kata ya Buhalahala wanatarajia kuwa na ofisi yao mpya ifikapo Desemba mwaka huu, ambayo itawezesha uendeshaji mzuri wa shughuli za chama na kuwa chachu ya maendeleo katika kata hiyo.



Post a Comment

0 Comments