BILIONI 15 KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI 105 VYA MKOA WA SIMIYU

 



*BILIONI 15 KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI 105 VYA MKOA WA SIMIYU*


✳️✅Wateja 3,465 wataunganishwiwa huduma ya umeme

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA); tarehe 24 Oktoba 2024 imemtambulisha rasmi mkandarasi; kampuni ya CCC (Beijing) Industrial & Commercial Ltd; kampuni kutoka China, itakayotekeleza  Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye vitongoji 105 vya majimbo saba (7) ya mkoa wa Simiyu; Mradi utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili, kuanzia sasa.

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Kihongosi, amempokea rasmi, mkandarasi, kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd na kumuahidi ushirikiano wa kutosha ili atekeleze na kukamilisha Mradi kwa wakati.

Mhe. Kihongosi amesema mkoa wa Simiyu unamahitaji makubwa ya umeme kutokana na kuongezeka kwa viwanda vya vidogo na vya kati na kwamba hiyo ni fursa kwa Wananchi kukuza uchumi na maendeleo kwa ujumla.

“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwenye Sekta ya Nishati hususan umeme; nikitoa mfano kwenye usambazaji wa umeme kwenye vijiji, Simuyu vijiji vyote 470 vilishaunganishwa na huduma ya umeme na sasa tunapokea Mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 15.6 na ambao Wananchi zaidi ya 3,465 watanufaika”. Amesema Mhe. Kihongosi.

Katika taarifa yake ya awali; Msimamizi wa Miradi ya REA mkoa wa Simiyu, Mhandisi, Deusdedit Msanze amemwambia Mkuu wa mkoa wa Simiyu kuwa, Wakala wa Nishati Vijiji (REA) umekamilisha Miradi ya kusambaza umeme katika Vijiji vyote 470 vya mkoa wa Simiyu kupitia miradi ya REA I, REA II, REA III Mzunguko wa I na I kwa nyakati tofauti.

“Mradi huu unalenga kufikisha umeme katika Vitongoji 105 vya Majimbo 7 ya Uchanguzi ya mkoa wa Simiyu ambapo kila Jimbo ni vitongoji 15. Mradi huu umeanza kutekelezwa tarehe 3 Septemba, 2024 na utakamilika tarehe 2 Septemba, 2026 Chini ya mkandarasi CCC (BEIJING) INDUSTRIAL & COMMERCIAL CO.LTD.”

“Mkandarasi huyo ataunganisha umeme kwenye Vitongoji 105 na kuunganisha Wateja 3465 ambapo vitongoji katika Majimbo hayo ni kama ifuatavyo; Bariadi (Vitongoji 15); Maswa Mashariki (Vitongoji 15); Maswa Magharibi (Vitongoji 15); Itilima (Vitongoji 15); Meatu (Vitongoji 15); na Kisesa (Vitongoji 15). Gharama ya mradi ni Shilingi 15,690,142,642.68 (pamoja na VAT).” Amekaririwa, Mhandisi, Msanze.

Kwa upande wake, Bi. Carol Wang kutoka kampuni ya CCC (Beijing) Industrial and Commercial Ltd; amesema kampuni yao, imejipanga ili kukamilisha Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 105 vya mkoa wa Simiyu kwa wakati na kuongeza kuwa sasa kazi inayoendelea ni ‘mobilization’ ya vifaa na Wafanyakazi ili kazi ya upimaji ianze.


Post a Comment

0 Comments