BUKOMBE WAUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS SAMIA, WAKABIDHIWA MITUNGI YA GESI

 






📌 *Mitungi ya Gesi 1500 Yatolewa Bure*


📌 *DC Bukombe Ahimiza Wananchi Kutumia Nishati Safi ya Kupikia na Kutunza Mazingira*

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Paskazi Muragili amesema kuwa Wilaya yake imeendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  kupitia kampeni yake ya kuhamasisha matumizi  ya nishati safi ya kupikia inayolenga kulinda afya na kutunza mazingira miongoni mwa Watanzania.

Akizungumza leo Oktoba 10, 2024 wilayani Bukombe mara baada ya semina ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi, Mhe. Muragili amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kuwatumikia Watanzania ikiwa ni pamoja na kuendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“ Moja ya changamoto zinazoleta athari ya afya na kusababisha vifo kwa akina mama ni matumizi ya nishati isiyo safi mfano kuni na mkaa ambavyo vinatoa hewa isiyofaa na  akina mama wa Tanzania  wamekuwa wakiathirika kwa kuvuta hewa hiyo lakini pia ukataji miti unaharibu mazingira yetu,” amesema Mhe. Muragili.

Amefafanua kuwa asilimia 78 ya Wilaya ya Bukombe ni misitu na asilimia 22 ni eneo la kuishi binadamu  ambapo kwa sasa misitu imeharibiwa kwa kiasi ilkikubwa kwa sababu ya ukataji miti  ikiwemo Msitu wa Taifa wa Kigosi.

“ Vyanzo vya maji navyo vinekuwa vikiharibika na ndio maana Rais Mhe. Dkt. Samia amekuja na mpango huu wa kugawa gesi kama leo tunavyogawa mitungi hii ya  gesi kwenu na mkaitumie. Aidha, tuna vijiji 64 ambavyo vyote vina umeme na mwaka wa fedha 2024/25 vitongoji 62 vitapata umeme na hivyo mtaweza pia kutumia majiko ya umeme ili kufikia malengo ya Serikali ya asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia ikifapo 2034,” amesema Mhe. Muragili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati  Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa REA imepewa  jukumu la kuhakikisha bidhaa za nishati safi za kupikia zinafika katika kila pembe ya nchi ili kumuwezesha kila mwananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama.

"Serikali kupitia REA imetoa ruzuku kwa bidhaa zote za nishati safi za kupikia lengo ikiwa ni kuhakikisha hakuna mwananchi anaachwa nyuma na Serikali imeingia makubaliano na watoa huduma ya kusambaza mitungi na katika kila wilaya ambapo kwa awamu hii kiasi cha mitungi 3,255 itatolewa kwa bei ya ruzuku katika kila Wilaya,” amesema Mhandisi Mwijage.

Aidha, Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa katika Wilaya ya Bukombe, mtoa huduma atakayesambaza mitungi ni Kampuni ya Manjis ambapo mitungi hiyo ya kilo sita ikiwa kamili na vichomeo vyake itatolewa kwa shilingi 17,500 tu ambayo ni nusu bei.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya  Wilaya Bukombe, Mhe. Yusuph Yusuph amesema kuwa  uwepo wa semina hiyo ya matumizi ya nishati safi ni muhimu kwa kuwa inalenga kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu za kuwahamasisha wananchi wa Bukombe kutumia nishati safi ili kuepuka madhara yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi.

Awali wananchi kutoka kata 17 za Wilaya ya Bukombe wamehudhuria semina ya matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyolenga kuhamasisha  wananchi juu ya matumizi yake na kuepusha athari zinazotikana na matumizi ya nishati isiyo safi.

Sambamba na semina hiyo ambapo wananchi hao walipata fursa ya kuuliza maswali kuhusu namna ya kutumia mitungi ya gesi, pia walipewa elimu kuhusu manufaa ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kunufaika na fursa za mfuko huo kwa jamii.








Post a Comment

0 Comments