RAIS MWINYI:TUENDELEE KUIOMBEA NCHI IDUMU KATIKA AMANI.

 




Na mwandishi wetu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza masheikh kutumia mikusanyiko ya kiimani kuiombea nchi amani ili Serikali iendelee na mipango ya maendeleo.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 25 Oktoba 2024 alipofungua Ijitimai ya Sita katika Msikiti wa Fissabilillah Tabligh Markaz, Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha , Alhaj Dk. Mwinyi ameeleza kuwa bila ya kuwepo kwa amani, hakuna jambo linaloweza kufanyika na kufikia malengo ya nchi.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amewasisitiza viongozi, masheikh, na waumini wa dini ya Kiislamu kuendelea kuhubiri amani, maadili, na tabia njema ili kujenga jamii bora.

Alhaj Dk. Mwinyi ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja kusisitiza jambo hilo, na wala si la kuwaachia masheikh na maamiri pekee yao.

Alhaj Dk. Mwinyi ameipongeza Jumuiya ya Fissabilillah Tabligh Markaz kwa kuendeleza Ijitimai kwa mafanikio makubwa kila mwaka na kuahidi kuwa Serikali itaunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi amewanasihi viongozi wa dini kutojiingiza kwenye siasa na mambo yaliyo nje ya misingi ya Uislamu.

Akitoa salamu za Jumuiya ya Kiislamu ya Fissabilillah Tabligh Markaz Zanzibar, Sheikh Kassim Saleh ameielezea hali ya amani nchini na kasi ya maendeleo iliyofikiwa Zanzibar kama matokeo ya kuwa na Rais mcha Mungu na anayejali watu wake.









Post a Comment

0 Comments