SERIKALI YAWAHIMIZA VIJANA KWENYE SAYANSI,MAHUNDI AFUNGUKA.

 


Na mwandishi wetu

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tanzania imesaini makubaliano ya uwekezaji na mafunzo na Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki ya China (CECIS LTD) kwa lengo la kuongeza ujuzi kwa vijana katika utengenezaji kompyuta.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kusaini makubaliano hayo Naibu Waziri wa Wizara hiyo Marryprisca Mahundi amesema Uwekezaji huo utaongeza ujuzi kwa vijana na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utengenezaji wa kompyuta Duniani.

Ameongeza kuwa kupitia Uwekezaji huo Tanzania inakwenda kupiga hatua kubwa katika masuala ya uchumi wa kidijitali ambako ndiko Duniani ilipo kwa sasa hivyo ili nchi ipige hatua ipo haja ya kuwekeza zaidi kwenye sekta ya Teknolojia.

Hata hivyo amesema Makubaliano hayo ni matokeo ya ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini China aliyoifanya hivi karibuni ambapo Kampuni hiyo ni wabobezi wa masuala ya usalama wa mitandao hivyo elimu waliyonayo itawawezesha vijana kujifunza na kupata wataalam wengi zaidi wa TEHAMA.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla amesema kupitia makubaliano hayo, zaidi ya makampuni 600 ya vifaa vya kompyuta yatawekeza Tanzania.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo pia utatoa fursa kwa watanzania hususani vijana kujifunza na kupata ujuzi ambapo wataweza kujiajiri na kuajiri watu wengine.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya huduma za mawasiliano ya kielekroniki ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia wa Kamati ya Kampuni hiyo, Guo Zhaoping amesema uwekezaji huo umefuata misingi ya nchi za Tanzania na China na kwamba unalenga kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

“Kampuni yetu inafanya uwekezaji katika mambo makuu matano ikiwepo sekta ya kompuya na usalama wa mitandao ambapo pamoja na kufanya shughuli za kibiashara pia tunalenga kukuza uchumi wa kidijitali baina yetu na nchi zingine, kwa hapa Tanzania tutafanya kazi kulingana na mahitaji” amesema Zhaoping.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema pamoja na mambo mengine, pia wamekubaliana kuvutia makampuni mbalimbali ya Kielekroniki kuwekeza nchini ambapo mwaka 2025 kutakuwa na maonesho makubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kompuya Afrika ambapo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume yake watakuwa wenyeji wa maonesho hayo.

Makubaliano hayo yamesainiwa Oktoba 21/2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Abdulla na Mwenyekiti wa Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki ya China CECIS, Guo Zhaoping na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Marryprisca Mahundi.

Post a Comment

0 Comments