Na mwandishi wetu
*📌 Ahoji matumizi ya Shilingi milioni 159 nje ya bajeti Ujenzi wa Kituo cha Afya Msimbati*
*📌 Mkurugenzi wa Halmashauri na Wataamu watofautiana Majibu*
*📌 Aiagiza TAKUKURU Kufanya Uchunguzi Ujenzi wa Kituo cha Afya*
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Novemba 17, 2024 amefanya ziara Wilayani Mtwara na kukagua ujenzi wa miradi inayotekelezwa kwa fedha zinazotolewa na wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maendeleo kama njia ya kurejesha rasilimali kwa wananchi kupitia (CSR).
Akikagua Kiktuo cha Afya Msimbati, Dkt. Biteko ameeleza kutoridhishwa na matumizi ya fedha iliyokuwa imepangwa kutumika katika ujenzi wa kituo hicho na kupelekea ongezeko la kiasi cha shilingi milioni 159.
Kituo hicho cha Afya awali kilikadiriwa kujengwa kwa gharama ya shilingi milioni 600 lakini gharama za ujenzi huo ziliongezeka hadi kufikia shilingi milioni 759 na hivyo kuibua maswali ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara, Abeid Kafunda amekiri kuwa hajui sababu za ongezeko la gharama hizo.
Aidha, Dkt. Biteko ameiagiza Taasisi ya Kuthibitj na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Mtwara kufanya uchunguzi wa kina kuhusu sakata la Kituo cha Afya cha Msimbati baada ya kubaini kuwa ujenzi wa mradi huo hauendani na thamani halisi ya fedha pamoja na kuchukuliwa hatua kali kwa wahusika wote wa usimamizi Mradi na kusababisha ongezeko kubwa la fedha tofauti na maeneo mengine nchini ambayo vituo vya Afya vinajengwa kwa thamani ya shilingi milioni 500 hadi 600.
Baadae, Dkt. Biteko alifanya ukaguzi wa majengo ya Kituo cha Afya Msimbati ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98 na kuwataka watekelezaji wa miradi mbalimbali nchini kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia kwamba miradi hiyo inakusudiwa kuwanufaisha Watanzania na sio vinginevyo. amesema Dkt. Biteko
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala amesema uongozi wa Mkoa umekuwa ukifanya ziara ya kukagua miradi hiyo inayojengwa kutokana na utekelezaji maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara inakotoka gesi wananufaika na rasilimali hizo kupitia CSR.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt. Biteko amekagua ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Msimbati ambacho kimekamilika na maombi ikiwa ni ujenzi wa Uzio, samani, mifumo wa ya TEHAMA na, maji nyumba ya makazi ya Mkuu wa Kituo.
Wakazi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara wamekuwa na kilio cha muda mrefu wakiomba huduma za maendeleo kutokana rasilimali ya gesi kuchimbwa katika mikoa hiyo suala lililoisukuma Serikali kuagiza TPDC kutoa fedha kupitia CSR ili iweze kunufaisha wananchi kama inavyotokea katika maeneo mengine ya Nchi.
Kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alielekeza kujengwa kwa kituo cha Afya katika eneo la Msimbati, Kituo cha Polisi pamoja na Uwekaji wa taa za Barabarani katika eneo hilo.
0 Comments