Na mwandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa Uongozi wa msikiti Mkuu wa Ijumaa- Utende kuimarisha darasa kwa watoto na Vijana ili kujenga chemchem ya maarifa sahihi ya dini ya kiislamu bila kujenga sura ya harakati na mitafaruku kwenye jamii.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo mapema leo Jumapili Novemba 17, 2024 wakati wa uzinduzi wa msikiti Mkuu wa Ijumaa- Utende wilayani Mafia mkoani Pwani, Msikiti uliojengwa na Taasisi ya Al-Jaziira Islamic Centre, akitaka msikiti huo kutumiwa vyema katika kuendesha na kurithisha mifumo adilifu ya Maisha kwenye jamii.
'Msikiti usimamiwe kwa maudhui ya kuiwema jamii inaouzunguka kukumbushana kumcha Mungu kwa kufuata kitabu chake cha Quran Takatifu pamoja na kufuata mafunzo aliyokuja nayo Mtumule wetu Muhammad (SAW) kwa kutakabali mfumo na mwenendo wa maisha yake."amesema Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa pia amewataka wadhamini wa msikiti huo kufanya tafiti na kuanzisha taasisi za elimu na mafunzo kwa vijana wa kike na wa kiume na watu wazima na kujenga mawasiliano na mahusiano na misikiti mingine ili kubadilishana maarifa ya dini na maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanayolenga kuendeleza jamii.
Waziri huyo wa TAMISEMI ametumia hadhara hiyo pia kutoa wito kwa watanzania wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024 ili kuweza kuwachagua viongozi wenye sifa zinazostahili na watakaowatumikia kwa uadilifu, akiwataka pia kuepukana na vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.
Katika tukio hilo lililohudhuriwa pia na Viongozi wa serikali na Chama wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge na Mkuu wa wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo, Mhe. Mchengerwa pia ametumia nafasi hiyo pia kuomba wananchi kuendelea kuiombea Kariakoo na waathirika wa janga la kuporomoka kwa Jengo la Ghorofa nne lililopo Kariakoo Jijini Dar Es salaam.
0 Comments