RAIS MWINYI AKUTANA NA UONGOZI WA KAMPUNI YA WUHAN

 



Na mwandishi wetu


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika ziara yake nchini China leo amekutana na ujumbe kutoka Kampuni ya Wuhan Guangfu Tangyuan Buer Cultural Development. Ujumbe huo ulifika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Westin, Shanghai, wakiwa na mwenyeji wao, Bwana Wenbao Tan, Mkurugenzi Mkuu kutoka Shirika la China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center.

Kampuni ya Wuhan Guangfu Tangyuan Buer Cultural Development, inayojishughulisha na kukuza na kuboresha utamaduni wa Kichina, uwekezaji katika utalii, uandaaji wa matamasha ya sanaa, utamaduni, na ubunifu wa kidijitali, imeonesha nia ya kuwekeza Zanzibar kupitia mradi wa China-Africa Cultural Exchange Industrial Park.

Mradi huo, wenye lengo la kubadilishana tamaduni, utakuwa na vituo vya Muziki, Kazi za Mikono, Uchoraji, utamaduni wa makabila mbalimbali, pamoja na utamaduni wa jadi kutoka China.

Rais Dk. Mwinyi amemuahidi Bwana Wenbao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kutoa ushirikiano kupitia Taasisi ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA). Naye, Bwana Wenbao Tan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center, amemueleza Rais Dk. Mwinyi utayari wao kutembelea Zanzibar na ujumbe wake mwezi Desemba 2024.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Saleh Saad Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Juma Burhan, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.







📅 05 Novemba 2024


📍Shangai, China

Post a Comment

0 Comments