WABUNIFU WA MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI WATAKIWA KUWA WELEDI KAZINI

 


Na mwandishi wetu

SERIKALI imewataka wataalamu wa ubunifu wa majengo na ukadiriaji majenzi kuwa weledi kazini badala ya kuangalia maisha yao binafsi ya kujipatia fedha kwa muda mfupi.

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 29, 2024 Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala , Edward Mpogolo akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko katika Mkutano wa  tano wa Bodi ya wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi.

Hata hivyo DC Mpogolo amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kufanyia maboresho sera ya Ujenzi ili kukuza sekta ya mabunifu Majengo na Wakadiriaji  Majenzi kufanya kazi kwa ufanisi na miradi ya ujenzi wanayopatiwa na Serikali na sekta binafsi kukamilika kwa wakati.

"Baadhi ya wataalamu wa ubunifu wa Majengo na ukadiriaji Majenzi wamekua wakiangalia maisha yao binafsi kwa ajili ya kujipatia fedha kwa muda mfupi huku suala la weledi kazini likiwa limewekwa pembeni hali ambayo inasababisha majengo kuwa chini ya kiwango.

Amesema kwasasa serikali ipo kwenye mchakato wa kufanyia maboresho sera ya ujenzi ili kutengeneza Sheria ya ujenzi itakayosaidia  wataalamu hao kufikia matamanio ya kukuza sekta ya ujenzi kutokana na mabadiliko ya teknolojia yanayoenda kwa kasi Duniani.

“Jitihada zinazopatikana katika sekta ya ujenzi inatokana na nyinyi wataalamu wa ubunifu wa Majengo na ukadiriaji Majenzi,ukiona mafanikio yaliyopo kwa sasa yanatokana na nyinyi,hivyo kwa niaba ya serikali  nawaomba sana muwe Wazalendo ili tumuunge mkono Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan” amesema DC Mpogolo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt Daudi Kondoro ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania( TBA) amesema kuwa watendaji wa Wizara wataendelea kusimamisha sekta ya wataalamu wa ubunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi ili waweze kua na weledi katika kazi zao.

“Wizara ya ujenzi itatenga fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa mafunzo wataalamu 180 Kila Mwaka ambao wanahusika na bunifu wa Majengo na ukadiriaji Majenzi,ili waweze kuwa na uelewa Moana katika taaluma yao” amesema Dkt.Kondoro.

Na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi wa wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji majenzi (AQRB) Dkt Ludigija Bulamile amesema kuwa kwa sasa Bodi hiyo imesajili 1586 ambapo kati yao 33 ni wageni kutoka nje ya nchi.

Mkutano huo wa tano wa Bodi ya wabunifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi(AQRB) umeenda sambamba na mahafali ya kwanza ya wahitimu wa mafunzo ya taaluma ya wabunifu Majengo na wadiriaji Majenzi ,ambapo zaidi ya wahitimu 130 wamehitimu na kutunukiwa vyeti na mgeni rasmi.

Post a Comment

0 Comments