Na mwandishi wetu
BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeidhinisha matokeo ya mitihani ya 100 ya bodi hiyo iliyofanyika Novemba, 2024 ambapo ufaulu umeeongezeka kutoka asilimia 66.4 kwa mwaka uliyopita na kufikia asilimia 70.3 na wanaume wakiongoza kwa ufaulu wa mitihani hiyo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA. Pius A. Maneno imeeleza kuwa watahiniwa waliofanya mitihani hiyo walikuwa 6,908 sawa na asilimia 91.3 kati yao wanaume walikuwa 3,802 na wanawake walikuwa 3,764 huku watahiniwa 658 sawa na asilimia 8.7 hawakufanya mitihani kwa sababu mbalimbali.
Aidha, kati ya watahiniwa 6,908 waliyofanya mitihani hiyo, watahiniwa 4,858 sawa na asilimia 70.3 wamefaulu mitihani yao ambapo watahiniwa 1,282 sawa na asilimia 18.6 wamefaulu masomo yote katika ngazi husika, hivyo wamestahili kupatiwa barua za ufaulu.
Watahiniwa wengine 3,576 sawa na asilimia 51.7 wamefaulu baadhi ya masomo katika ngazi husika na watahiniwa 2,050 waliobaki sawa na asilimia 29.7 hawakufaulu mitihani yao.
Bodi ya NBAA, inawapongeza wale wote waliofuzu mitihani yao na kuwataka wale ambao hawajafuzu kutokata tamaa bali waongeze bidii zaidi katika masomo yao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani ijayo ya bodi.
Hivyo, Bodi inawashauri kuendelea kutumia vema vitabu vilivyotayarishwa na bodi katika kujiandaa kwa mitihani yao kwa kusoma vitabu vingine vya ziada ili kuongeza ufahamu zaidi katika masomo hayo.
0 Comments