-Wajadili hali ya usalama katika Soko la Kariakoo.
-Aeleza dhamira ya Mkoa kuwa na mpangilio mzuri wa wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Disemba 21, 2024 amekutana na wadau mbalimbali wa Biashara katika eneo la Kariakoo pamoja na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO, TANROAD, LATRA, DAWASA, Taasisi za fedha na Kamati ya Usalama ya Mkoa
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimejadili maswala mbalimbali yenye lengo la kuboresha ufanyaji biashara Kariakoo unaokidhi viwango vya kimataifa hususani hali ya usalama ambayo itawezesha biashara kufanyika saa 24, ambapo RC Chalamila ameipongeza Halmashauri ya Jiji kwa kuanza mchakato wa ununuzi wa Camera ambazo zinatarajiwa kufungwa maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kariakoo.
Aidha Katika kupunguza msongamano kwenye eneo la kariakoo RC Chalamila amesema kupitia kikao hicho wamejadili mpango maalum shirikishi wa kuzuia aina zote za magari,bajaji na pikipiki kuingia katikati ya mitaa ya soko la kariakoo wakati wa asubui, mchana na jioni.
Vilevile RC Chalamila amesema eneo la kariakoo ni muhimu kibiashara linahudumia Tanzania na nchi jirani hivyo magari yataruhusiwa kuingia nyakati za usiku pekee ili kupunguza msongamano na kuruhusu biashara kufanyika bila usumbufu asubuhi hadi jioni
Sambamba na hilo Mhe Mkuu wa Mkoa amesema ifike wakati Kariakoo iwe ni "Special Zone ya Kibiashara" mtu akitaka kufanya biashara lazima awe amekidhi vigezo vitakavyowekwa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara na wadau wengine ikiwemo taasisi za fedha kuona namna ya kuongeza muda wa kufanya kazi hadi usiku hususani katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi
Sanjari na hilo amelitaka jeshi la polisi kuimarisha ulinzi kwa wafanyabiashara na wananchi katika kipindi hiki cha sikukuu ambapo amesema kwenye kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka uhitaji wa bidhaa mbalimbali huongezeka kwa wananchi hivyo mpango huu wa kuongeza muda wa kufanya kazi utawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.
0 Comments