TFRA Yatakiwa Kuandaa Mpango wa Kuongeza Matumizi ya Mbolea Nchini


Na mwandishi wetu

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Omary, ametoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuandaa mpango mahsusi wa kuongeza matumizi ya mbolea ili kuimarisha sekta ya kilimo nchini. Wito huo ulitolewa hivi karibuni wakati wa ziara yake katika ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo alikutana na menejimenti ya Mamlaka hiyo.

Katika kikao hicho, Dkt. Hussein alipokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Aidha, aliagiza TFRA kuandaa mwongozo wa biashara ya mbolea na uwekezaji, ili kufanikisha azma ya taifa ya kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ifikapo mwaka 2030.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Kilimo kuhakikisha usimamizi bora wa mbolea, kuhamasisha uwekezaji endelevu katika sekta ya kilimo, na kuchochea tija kwa wakulima kupitia upatikanaji wa mbolea bora na ya kutosha.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, aliainisha mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo. Alisema TFRA inahusika na kudhibiti ubora wa mbolea zote zinazotumika nchini na zinazouzwa nje ya nchi, pamoja na kufuatilia na kukusanya takwimu za uwepo na usambazaji wa mbolea nchini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi, kufikia tarehe 30 Novemba 2024, jumla ya tani 769,061 za mbolea zinapatikana nchini sawa na 77% ya mahitaji ya mbolea  ya tani 1,000,000 kwa msimu  wa kilimo 2024/25. Kiwango hiki kinatokana na bakaa ya msimu uliopita (tani 260,403), uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi (tani 58,669), na mbolea iliyoigizwa kutoka nje ya nchi tani 449,988.

Alieleza kuwa, kati ya mbolea iliyoingizwa nchini, jumla ya tani 63,006 zimeuzwa nje ya nchi na  tani 706,055 zimebaki  kwa ajili ya matumizi ya ndani, ambayo ni sawa na 70.61% ya mahitaji. 

Mkurugenzi Laurent  alieleza kuwa, hadi kufikia Novemba 30, 2024, kiasi cha tani 350,174 kipo nchini tayari kwa matumizi mwanzoni mwa msimu wa kilimo wa 2024/25. Mbolea iliyopo nchini ni pamoja na tani 94,986 za Urea, tani 15,318 za DAP, tani 57,793 za SA, tani 43,158 za CAN, na tani 19,637 za MoP.

Hali ya upatikanaji wa mbolea kwa msimu wa 2023/24 ilielezwa kuwa ni ya kuridhisha, na TFRA inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kuagiza mbolea zaidi ili kufikia mahitaji ya wakulima kwa msimu wa kilimo wa 2024/25. Pia, wakulima wanahimizwa kununua mbolea mapema ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija zaidi.




 

Post a Comment

0 Comments