ULEGA ATOA WIKI MBILI WAKANDARASI MIRADI YA DHARURA WAWE SITE

 



Na mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ametoa wiki mbili kwa wakandarasi wote nchini waliopata ujenzi wa miradi ya dharura Contigency Emegency Response Component (CERC),kuanza kazi mara moja.

Amesema hayo leo wakati akikagua barabara ya Arusha-Holili ambayo iliathiriwa na mvua katika maeneo ya Kwamsomali na King'ori.

"Mhe. Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni 800 kwa ajili ya kazi hizo katika mikoa 22 nchini kote", amesema Ulega.

Amesema mkandarasi alieshindwa aondoke haraka sana kwani Wizara haita mvumilia mkandarasi asiekwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya sita.

" Wakandarasi mliopata miradi ya dharura amkeni  mfanye kazi usiku na mchana", amesisitiza Ulega.

Katika hatua nyingine Waziri Ulega amesema katika kukabiliana na msongamano wa magari mijini Serikali itaboresha barabara ya Arusha-Holili iwe  njia nne ambapo awamu ya kwanza itahusisha sehemu ya Tengeru-Usa river km 11.35 mkoani Arusha na Mailisita- Kiboriloni km 11.3 mjini Moshi pamoja na ujenzi wa daraja jipya la Kikafu.

"Ujenzi huu unaolenga kupunguza msongamano katikati ya miji uendane na uwekaji taa za barabarani ili kupendezesha miji," amesisitiza Waziri Ulega.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu ameipongeza Wizara ya ujenzi na TANROADS kwa kazi nzuri ya ujenzi wa barabara mkoani humo.

"Hii barabara ya Arusha Holili ni muhimu kwa utalii na uchumi wa mkoa wetu hivyo upanuzi wake ukiwa njia nne utaleta tija kwa mkoa wetu", amesema Babu.

Nae Mbunge wa Hai Saashisha Mafue amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi ya maendeleo mkoani humo ikiwemo ya barabara.








Post a Comment

0 Comments