#Hali ya upatikaji wa barabara na madaraja yafikia 19%
Kibaya ,Kiteto
WANANCHI wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ambao utasaidia kufungua uchumi wa wilaya hiyo.
Wakizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo wananchi hao wamesema awali kabla ya ujenzi wa miundombinu hiyo walikuwa wakikumbana na changamoto za usafiri na usafirishaji bidhaa na mazao mbalimbali yanayolimwa wilayani humo jambo lililochangia kuzorota kwa ukuaji wa uchumi wao.
Bw. Jafari Hassan ambaye ni dereva wa bodaboda Mkazi wa Kijiji cha Mbeli katika Kata ya Mbeli wilayani humo anasema awali alikuwa akikumbana na changamoto katika shughuli zake za usafirishaji kabla ya kujengwa kwa daraja linalounganisha kata hiyo na maeneo mengine lakini kwa sasa anafurahia kazi yake baada ya kujengwa kwa daraja hilo la mawe.
“Kwa sasa tuna ‘enjoy’, tulipata shida sana kwa kukosekana kwa hili daraja hususani sisi bodaboda, tulipata changamoto kubwa kusafirisha akina mama kwenda kliniki mpaka tunaamua kupita ng’ambo lakini kwa sasa tunamshukuru Mungu kwa kupata daraja zuri kama hili na sasa tunapita juu, kwa kweli daraja hili limeturahisishia sana tunaishukuru Serikali na viongozi wetu wametukamilishia daraja ni jambo jema sana.” Alisema Jafari.
Naye, Bw. Bakari Kilama, Mkazi wa Mji mdogo wa Matui wilayani humo anasema hapo awali hakukuwa na barabara nzuri kiasi ambacho wakazi wa mji huo walikuwa wakipita kwenye njia ambazo magari yalikuwa yakipasua kwa kupita ndipo na wao wapite ukilinganisha kwa sasa baada ya kujengewa barabara ya uhakika pamoja na mitaro.
Amesema kwa kiwango kikubwa shida hiyo imepungua na sasa wanaweza kusafirisha mazao yao kutoka katika mji huo na kuyapeleka maeneo mengine kwaajili ya biashara jambo ambalo limewanufaisha kiuchumi.
“Kwanza zamani hakukuwa na barabara yaani ilikuwa tu watu wanapita kwenye mapalio ambayo magari yanapasua yenyewe, lakini kwa mradi huu ambao wamekuja kututengenezea hizi barabara tunashukuru kwa sababu kwa kiwango kikubwa tabu imepungua ya kusafirisha mazao yetu kutoka hapa kwenda sehemu nyingine, imekuwa kidogo ni rahisi, kwa hiyo sisi wananchi wa hapa tumenufaika kwa hili.” Alisema Bakari.
Kwa upande wake Bw. Siraji Ally ambaye ni Mkazi wa Matui anasema amefurahi baada ya kupelekwa mradi wa barabara mjini humo ambapo hapo nyuma walikuwa wakipata shida hasa watoto wa shule walikuwa wakishindwa kuhudhuria vipindi vya masomo kutokana na wingi wa maji yaliyokuwa yakituama jambo lililosababisha kuzorota kwa elimu katika mji huo lakini kwa sasa baada ya ujenzi wa barabara na mitaro hali imekuwa shwari.
Siraji ameipongeza Serikali kupitia Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) na kusema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo imewarahisishia kusafirisha mazao yao ikiwemo mahindi, alizeti, karanga na mbaazi baada ya magari kuweza kufika katika mashamba yao na hivyo kukua kwa mzunguko wa biashara katika mji huo.
“Barabara ni kitega uchumi, kwa sababu bila barabara maendeleo hakuna, maana yake utatoa mazao hapa utapeleka sehemu nyingine kama huna barabara nzuri, lakini kama barabara sio nzuri sio rafiki huwezi kupeleka mazao sehemu nyingine. Kwa hapa tunashukuru kwa sababu mazao sasa yanatolewa hapa yanapelekwa sehemu nyingine, kwa hiyo mzunguko wa biashara unakuwepo.” Alisema.
Akizungumzia kuhusu miradi ya Barabara na madaraja wilayani humo Meneja wa Tarura Wilaya ya KIteto, Mhandisi Edwin Magiri amesema Tarura inahudumia mtandao wa Barabara wenye jumla ya Kilometa 1,291.137, kati ya hizo Kilometa 200.3 ni changarawe, Kilometa 5.128 barabara za lami na Kilometa zaidi ya 1,014 ni barabara za vumbi.
Mhandisi Magiri amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Bajeti ya shilingi Bilioni 2.8 kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 kutoka Bajeti ya shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu wilayani humo ambayo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 na kufanya hali ya upitikaji wa barabara na madaraja wilayani humo kufikia asilimia 19 kutoka 11 ya awali.
“Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejenga zaidi ya madaraja 18, kwa hiyo madaraja ya teknolojia ya mawe tumeyajenga katika maeneo mbalimbali ambayo gharama zake ni nafuu kidogo ukilinganisha na yale madaraja ya zege,” Alisema na kuongeza,
“Awali tulikuwa na Bajeti ya Bilioni 1.684 ambayo tulipata kutoka kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, lakini baada ya hapo tukaenda kwenye Bajeti ya Bilioni 1.3 kabla ya awamu ya sita, lakini baada ya awamu ya sita Bajeti ya uhakika ambayo tunayo ni Bilioni 2.8 kwa hiyo ni ongezeko la zaidi ya silimia 100.” Alisema Mhandisi Magiri
Aidha, amesema licha ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo, lakini pia wanatoa rai na elimu ya mara kwa mara kwa wananchi wa Kiteto kuhusu kuitunza miundombinu hiyo ambayo Serikali imetoa fedha nyingi kuijenga ili iweze kudumu kwa manufaa yao.
0 Comments