WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA SHILINGI YA TANZANIA KUUZA NA KUNUNUA BIDHAA NCHINI

 


Na mwandishi wetu

Benki Kuu ya Tanzania imewataka wananchi wote kutumia Shilingi ya Tanzania wakati wanapofanya miamala yao nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Januari 8, 2025, Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema ni kosa kununua, kuuza bidhaa na huduma hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni.

Amesema kutumia fedha za kigeni kufanya miamala ya ndani ni kuhujumu uchumi wetu na kunufaisha sera ya fedha ya nji za kigeni.

Gavana Tutuba amesema Benki Kuu itaendelea kusimamia utekelezaji wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, 2006 kinachohimiza matumizi ya Shilingi katika kufanya miamala hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyokuwa ya lazima.

Gavana Tutuba ameyasema hayo wakati akizungumza na wakuu wa benki na taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari wakati akitangaza uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha kwamba Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu itabakia kuwa asilimia 6, kama ilivyokuwa katika robo mwaka iliyopita.

Amesema uamuzi huo ambao ulifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo iliyokutana tarehe 7 Januari 2025 jijini Dar es Salaam umefikiwa kutokana na tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini.

Kiwango hiki cha Riba ya Benki Kuu kinatumika wakati benki zinapofanya biashara ya fedha kati yao.

Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema hadi hivi sasa, Benki Kuu imeshanunua tani 2.5 za dhahabu ikiwa ni jitihada zake za kuongeza akiba yetu ya fedha za kigeni.

Lengo ni kununua tani 6 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25.



Post a Comment

0 Comments