WAZIRI ULEGA AMBANANISHA MKANDARASI BARABARA YA TUNGAMAA - MKANGE, MKANDARASI AOMBA RADHI AJIPANGE UPYA.
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta kumpa ripoti ya kitaalam kuhusu kasi ya ujenzi usioridhisha kwa Mkandarasi M/s China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara ya Tungamaa-Mkwaja-Mkange Km 95.2 ambayo ni sehemu ya barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo ili achukue hatua stahiki.
Akizungumza mjini Pangani leo Waziri Ulega amesema haridhishwi na kasi ya mkandarasi huyo anayejenga sehemu ya tatu ya barabara hiyo kwa kuwa asilimia 40 badala ya 90 huku muda wa kukamilisha kazi ukiwa umebaki miezi mitatu.
"Haikubaliki na haivumiliki kutoa visingizio vya mvua wakati wakandarasi wengine wanafanya vizuri katika maeneo hayo hayo", amesema Ulega.
Aidha Waziri Ulega amempongeza Mkandarasi Shandong anayejenga daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 kwa kazi nzuri na kumtaka kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha daraja hilo kwa wakati.
"Asilimia ya daraja inaridhisha ongezeni bidii,wataalam na muda wa kufanya kazi ili muwe mbele ya muda na barabara unganishi km 14.3 nazo zikamilike" amesisitiza Ulega.
Kuhusu mkandarasi CHICO anayejenga sehemu ya kwanza ya Tanga-Pangani KM 50, Waziri Ulega amesema kwamba tayari Serikali
imeshamlipa Mkandarasi huyo Shilingi Bilioni 4.7 ili kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Pangani Jumaa Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa daraja hilo na kusisitiza ujenzi huo utaongeza shughuli za kiuchumi mkoani Tanga, Pwani na ushoroba wa Bahari ya Hindi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Batilda Buriani ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa Barabara ya kimkakati ambapo inaunganisha nchi jirani ya Kenya na mikoa ya Tanga,Pwani na Dar es salaam na kusisitiza wananchi kutumia fursa za miradi hiyo kukuza biashara na kuibua fursa za ajira.
Barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo ni sehemu ya barabara kuu ya ushoroba wa pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Malindi-Mombasa hadi Lungalunga nchini Kenya na Horohoro-Tanga-Pangani-Bagamoyo hadi Dar es salaam nchini Tanzania ambapo kwake kutakuza Uchumi, Utalii na Biashara.
0 Comments