Mwanasheria Mkuu: Tunamshukuru Rais Samia kwa kukilea PBA

 


NA MWANDISHI WETU

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Hamza Johari amesema wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akikilea Chama cha Mawakili wa Serikali nchini (PBA), na kukiwezesha kuwa imara.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ametoa pongezi hizo, leo Aprili 14, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa PBA ambao ni wa tatu, uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Alisema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inasema, "Utawala wa Sheria katika utekelezaji wa majukumu ya serikali ni nguzo muhimu katika kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo  2050" 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johari," Amesema, "Kaulimbiu hii inatukumbusha namna bora ya ufanyajikazi kwa weledi na tayari imeshatengenezwa mpango mkakati ambao utatekelezwa kwa moyo na hali ya juu na pia ni mpango unaoishi na kila baada ya muda tutakuwa tunaitana kujitathmini tulipofikia."

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johari amewataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanatumia ipasavyo kliniki za ushauri wa Sheria kwa kutoa elimu ya sheria zilizopo katika ngazi za mikoa na wilaya katika kutoa elimu ya masuala husika kwa jamii.

Pia ameiomba Serikali kuendelea kuiongezea bajeti Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali amesema kumekuwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti katika ofisi yake pamoja na vitengo vyake hasa katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, jambo ambalo limekuwa likiathiri kliniki za kisheria katika mikoa na wilaya.

Post a Comment

0 Comments