Na mwandishi wetu
Wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani wamekaribishwa kushiriki tamasha kubwa la muziki wa injili lijulikanalo kama Mtoko wa Pasaka, litakalofanyika Aprili 20, 2025 katika Ukumbi wa Superdome, Masaki kuanzia saa saba mchana.
Tamasha hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa mwimbaji mkongwe wa muziki wa injili, Christina Shusho, na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, chini ya Mwenyekiti wake Steve Mengele maarufu kama Steve Nyerere, likilenga kuwakutanisha Watanzania na kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa njia ya maombi na nyimbo za injili kutoka kwa waimbaji mbalimbali wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Steve Nyerere alisema kuwa tamasha hilo litakuwa la kipekee na litabeba kaulimbiu: “Kwa Maombi Utashinda.”
“Maombi yana nguvu kuliko mtutu wa bunduki, kuliko matusi, na kuliko kitu kingine chochote. Siku hiyo tutaliombea Taifa letu pamoja na Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema kwa msisitizo.
Steve alieleza kuwa mwezi wa Aprili umebeba uzito wa kiroho kwa imani mbalimbali, ikiwemo Ramadhani kwa Waislamu na Kwaresma kwa Wakristo, hivyo tamasha hili limepangwa kwa uangalifu ili kuendana na hali hiyo ya kiimani.
Mbali na burudani na maombi, Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao pia itatoa paketi za vifaa vya uzazi kwa ajili ya kusaidia akinamama wajawazito katika hospitali zote za wilaya jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Pasaka kwa vitendo vya huruma na huduma kwa jamii.
0 Comments