Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema kama kuna watu wanaoojifanya hawaoni ufanisi wa kazi na maendeleo yalioletwa na Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, macho yao huenda yakawa na uoni hafifu au ni watu hamnazo.
Chama hicho kimeeleza kuwa kwa watu makini wanaoijua Tanzania ilipotoka, ilioyapitia na mahali ilipo sasa, atakiri kazi kubwa ya kimaendeleo imefanyika kwa ustadi na viwango.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis , amesema maendeleo yaliochomoza Awamu ya sita yameishangaza dunia .
Mbeto alisema tokea Rais Dk Samia achukue kijiti cha uongozi kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya tano Marehemu Dk John Magufuli , Rais Dk Samia na Serikali yake wameitendea haki nchi na kutimiza wajibu kwa Taifa na watu wake .
Alisema licha ya kufanyika juhudi za kisera na kukamilika kwa miradi ya kimkakati ilioanzishwa katika awamu ya Dk Magufuli huku Dk Samia akiwa Makamo wa Rais, miradi yote imeimalizika na kuanzisha mingine na kukamilika.
"Walipotokea watu wazima na akili zao au kundi la wachache na kudai hakuna kazi yaliofanyika lazima kwanza umtazame mtu huyo kama ni timamu kichwani mwake. Vinginevyo watu hao watakuwa na uoni hafifu wa macho au ni watu hamnazo vichwani "Alisema Mbeto
Aidha, Katibu Mwenezi huyo alisema kwa Watanzania walioishi nje ya Nchi kwa miaka zaidi ya thelathini, wanapotembelea Wilaya na Mikoa, hukiri kuwa kazi kubwa ya nguvu imefanyika kwa kipindi kifupi .
"Chama chetu kwa asili ndicho kilichopigania Uhuru na kufanya Mapinduzi Zanzibar. Ndicho kinachojua jinsi nchi zetu wakoloni walivyoziacha , zilivyokuwa, mahali zilipo na yote yaliokwishafanyika ambayo hayakuwepo miaka sitini iliopita" Alieleza .
Mbeto alisema anapata tabu ya kuvilaumu vyama vilivyoanzishwa Mwaka 1992 kwa kushindwa kwao kupima hatua za Maendeleo zilizofikiwa kwa kuwa havikuwepo kabla ya Uhuru na Mapinduzi , ndio maana viongozi wake hubeza mafanikio yaliofikiwa.
"Tanzania Bara na Zanzibar kwa ujumla si zile wakati wa Mjerumani , Mwingereza na Sultan. Tanzania yetu sasa ndio nchi ya furaha na kujivunia . Yenye Amani na maendeleo makubwa ya kiuchumi "Alisisitiza Mbeto.
Akijigamba zaidi ,Katibu huyo Mwenezi alisema ni Tanzania ya leo ina watu wenye viwango vya elimu, Vituo vya Afya kata zote , hospitali za wilaya na mikoa zenye dawa matibabu pia kuinuka kwa Sekta za Kilimo , Utalii, Uvuvi , Barabara na Biashara .
"Haipo ile Tanzania ya kusafiri kwa basi siku tatu hadi nne toka Dar es salaam hadi Mwanza, Dodoma , Kagera au Kigoma. Haitarudi ile Tanzania ya mtumishi akihamishiwa kwenda Mikoa ya Mtwara , Ruvuma au Lindi yuko tayari kuacha kazi " Alisema Mbeto
0 Comments