CHAMA CHA NLD CHAONESHA UIMARA NA MSIMAMO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA

 


 

Na Ombe B. Kilonzo


Chama cha National League for Democracy (NLD) kimejidhihirisha kama miongoni mwa vyama makini vinavyojiandaa kwa weledi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Kupitia maandalizi ya mapema, NLD kimeweza kuweka msingi wa mshikamano wa ndani na kujiepusha na migogoro ya kawaida inayoyumbisha vyama vingi wakati wa uchaguzi.

Tayari miezi mitatu iliyopita, Chama cha NLD kilifanya uchaguzi maalum wa ndani ya chama kupitia Mkutano Mkuu Maalum. Zoezi hilo liliwezesha chama kuondoa makovu, migogoro na misuguano ya kawaida inayozuka miongoni mwa watia nia wa nafasi mbalimbali mapema. Kwa hatua hiyo, Chama cha NLD sasa kinaingia katika uchaguzi mkuu kikiwa imara, kikiwa chama kimoja chenye mwelekeo wa ushindi.

Hatua hii ni tofauti kabisa na hali ya vyama vingine, hasa vya upinzani, ambavyo bado vinahangaika kuponya majeraha ya uchaguzi wa ndani. Vyama hivyo vimejikuta vikikumbwa na makundi hasimu, lawama, na sintofahamu ya kiuongozi, hali inayopunguza kasi ya maandalizi yao kuelekea uchaguzi mkuu.

Baadhi ya makosa ya vyama vya upinzani yamekuwa ni kuiga ratiba ya uchaguzi ya chama tawala (CCM), jambo ambalo limechangia kuibua migogoro ya ndani ya vyama isiyokuwa ya lazima. Hali hiyo hupelekea vyama kupambana na wanachama wao badala ya kushindana na chama tawala katika uwanja wa sera na mikakati, hiyo ndio Strategic ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu.

Kwa upande wa Viongozi wa Chama cha NLD waliona hatari hii mapema. Mw/kiti wa chama hicho, Mfaume Khamis, na Katibu Mkuu Doyo Hassan Doyo, waliamua kupanga ratiba huru ya uchaguzi wa ndani iliyoendana na mazingira ya chama chao, na kufanya mkutano mkuu maalum wa Chama hicho tarehe 10/04/2025. Uamuzi huo umewaletea utulivu mkubwa ndani ya chama na kuwaweka wanachama kwenye mstari wa maandalizi ya uchaguzi kwa ari mpya.

Katika mahojiano mafupi, Katibu Mkuu Doyo alinukuliwa akisema “Sisi NLD tunaamini katika maandalizi ya mapema. Hatutaki kusubiri hadi dakika za mwisho ndipo tukimbie. Tumejifunza kutoka kwa wengine, na sasa tunatumia uzoefu huo kutengeneza historia yetu wenyewe.” Doyo Hassan Doyo.

Chama cha NLD kimesajiliwa rasmi kama chama cha siasa nchini Tanzania kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya kupitia sera zinazolenga maendeleo ya wananchi, uwajibikaji na usawa wa kijamii. Kikiwa miongoni mwa vyama vilivyosajiliwa na kupata usajili wa kudumu, NLD kimekuwa kikijijenga taratibu kwa msingi wa demokrasia ya ndani, ushirikishwaji na maono ya pamoja.

Kipindi cha nyuma, chama hiki hakikuweza kujitanua kwa kasi katika ngazi ya kitaifa, lakini sasa kinaonesha mabadiliko makubwa katika ushawishi na mikakati. Taarifa kutoka ndani ya chama zinaonesha kuwa tayari baadhi ya wanachama wameanza kutia nia ya kugombea nafasi mbalimbali za udiwani na ubunge nchi nzima, hali inayoashiria kukua kwa ushawishi na uimara wa chama hicho.

Kwa sasa, NLD kiko hatua ya mwisho ya mchakato wa kusimamisha wagombea wake wa udiwani na ubunge katika kila mkoa wa Tanzania. Hili ni jambo la kujivunia kwani ni miongoni mwa vyama vichache vilivyo tayari mapema kwa ushindani wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktober mwaka huu.

Katika juhudi za kuongeza ufanisi, Katibu Mkuu Doyo hivi karibuni alifanya ziara za kukabidhi vifaa vya chama kama vile bendera, kadi na nyaraka nyingine kwa wanachama katika baadhi ya mikoa, hatua ya kuimarisha matawi ya chama na kuwapa motisha wanachama kuelekea uchaguzi mkuu.

Hali hii inatofautiana sana na vyama vingine vya upinzani ambavyo bado vinajikongoja, licha ya kuwa na usajili wa kudumu. Wakati wengine wakianza kuamka kisiasa, Chama cha NLD tayari kipo mtaani, kikisambaza vifaa, kikihamasisha wanachama, na kujipanga kwa ajili ya kampeni za kitaifa.

Kwa ujumla, Chama cha NLD kimeonesha kuwa ni chama chenye mikakati, maono na uongozi makini unaojali uthabiti wa ndani na maandalizi ya muda mrefu. Huku wimbi la kisiasa likizidi kupanda kuelekea Oktoba, chama hiki kinazidi kuwa kielelezo cha nidhamu ya kisiasa na ushindani wa kweli.

Chama cha NLD kikiendelea kwa kasi hii, huenda kikaibuka kuwa mshindani wa kweli katika uchaguzi mkuu ujao, kikiwa sauti mbadala yenye misingi madhubuti ya maendeleo ya kitaifa. Katika siasa za Tanzania, Chama cha NLD kimethibitisha ya kwamba kipo tayari kuwaletea watanzania dira mpaya inayotokana na sera yake ya Uzalendo, Haki na Maendeleo. "Hakika Chama cha NLD kimesimama Imara Ki mkakati kwajili ya Maandalizi ya Mapema na ya Kipekee, kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025"

Nawasilisha.


Imeandikwa na.

Ombe B.Kilonzo

Mchambuzi wa Siasa na Maendeleo ya Jamii.

Post a Comment

0 Comments