Na. Ombe B. Kilonzo.
Hakika huu ni mwanzo mpya wenye kiwango kikubwa cha mafanikio ya haraka kwa Mhe. Doyo Hassan Doyo katika siasa.
Katika ulingo wa siasa za Tanzania, majina ya viongozi wenye uthubutu, maono na uthabiti wa msimamo wapo wachache mno, na moja ya majina yanayopata uzito huo kwa sasa ni jina la Mhe. Doyo Hassan Doyo, mwanasiasa ambaye safari yake ya kisiasa inaacha alama kila anapopita. Kuondoka kwake kutoka chama cha ADC na kujiunga na chama cha NLD si tu tukio la kawaida, bali ni kielelezo cha mabadiliko ya kweli na ujasiri wa kisiasa unaolenga mafanikio ya haraka, hasa mafanikio thabiti ya kisiasa.
Katika kipindi ambacho wanasiasa wengi hubaki katika vyama vinavyo wanyima faraja hata kama hawafurahishwi na mwenendo wa vyama hivyo kwa kuhofia kupoteza nafasi au ushawishi wao, Doyo aliamua kuchukua hatua ya kihistoria kwa kuondoka ADC na kujiunga na NLD. Hatua hii haikuwa ya kubahatisha, bali ya kimkakati, ikichochewa na kiu ya kutafuta uhuru zaidi wa kisiasa, mazingira bora ya kushughulikia masuala ya wananchi, na nafasi pana ya kujieleza kama mwanasiasa huru.
Mara baada ya kujiunga na NLD, Mhe. Doyo amekuwa chachu ya mageuzi ndani ya chama hicho. Kwa muda mfupi tu, ameweza kukijengea chama sura mpya, kukiimarisha katika medani ya siasa za kitaifa, na kukifanya kiwe miongoni mwa vyama vinavyotambulika na kuheshimiwa nchini. Mafanikio haya yanadhihirisha uwezo wake wa kiuongozi na weledi wa hali ya juu katika siasa za vyama vingi.
Mhe. Doyo haamini katika siasa za kubahatisha. Anaamini katika mipango, ujasiri na maono kila wakati, na hutumia ujasiri wake kama fursa ya kupambania haki yake ya kikatiba, hasa haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Katika hotuba na kauli zake, mara kwa mara hurejea kauli ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa taifa hili kuwa vyama si baba wala mama yetu, akisisitiza kuwa mwanasiasa ana haki ya kuchagua jukwaa bora zaidi la kutoa huduma kwa wananchi. Na kwa sasa, jukwaa hilo kwake ni NLD.
Katika muktadha wa sasa wa siasa za Tanzania, wananchi wengi, hasa wasiofuatilia siasa kwa karibu, wanamtambua zaidi Doyo wa NLD kuliko Doyo wa ADC. Hii ni kwa sababu mabadiliko aliyofanya yameleta matokeo ya haraka ndani ya NLD, matokeo yaliyo wazi na yenye mvuto kwa umma, jambo linaloongeza imani ya wananchi kwake.
Siasa ni sayansi, na kama ilivyo kwa sayansi nyingine, mafanikio yake hupatikana kupitia utafiti, uamuzi thabiti na uthubutu wa kubadilika kutokana na nyakati. Mhe. Doyo Hassan Doyo amethibitisha kuwa yeye ni mwanasiasa wa aina hiyo, mwenye uthubutu, maono na uelewa mpana wa mustakabali wa siasa safi katika taifa hili. Safari yake ndani ya NLD siyo tu mwanzo mpya, bali ni fursa ya kuandika historia mpya ya kisiasa nchini Tanzania.
Doyo wa NLD ni bora kuliko Doyo wa wakati wowote katika Medani za kisiasa.
By Ombe B. Kilonzo
0 Comments