SEKTA YA NISHATI YACHANGIA ASILIMIA 14.4 YA PATO LA TAIFA

 




*📌Kapinga ampongeza Rais, Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Nishati*


📌 *Aeleza mafanikio yaliyofikiwa katika Umeme, Gesi Asilia na Mafuta*


📌 *Asisitiza kuwa Nishati ni moyo wa uchumi*



Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Sekta ya Nishati ni moja kati ya Sekta tatu nchini ambazo zimechangia ukuaji wa pato la Taifa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2025.

Kapinga ameyasema hayo wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji Bungeni Jijini Dodoma. 

"Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia kwa tathmini kati ya mwaka 2024 hadi 2025 Sekta ya Nishati imefanya vizuri katika kuchangia pato la Taifa, Sekta hii imetoka asilimia 5.8 mwaka 2015 na sasa hivi tunazungumzia asilimia 14.4”. Amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, Sekta ya Nishati imeweza kufanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miradi

ambapo  amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa uwekezaji huo mkubwa.

"Katika Gesi na Mafuta yamepatikana mafanikio makubwa sana ikiwemo uendelezaji wa miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia, katika kitalu cha Mnazibay na Songosongo Serikali imeweza kuzalisha futi za ujazo bilioni 25.51 kwa kipindi cha miaka minne kwa kila kimoja. 

Ameongeza kuwa, Serikali imesaini mkataba katika kitalu cha Ruvuma Ntorya na sasa hivi kipo katika hatua za awali katika kuzalisha na kuendeleza gesi asilia.

Amesema katika kipindi cha miaka minne Sekta ya Nishati imepata mafanikio makubwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ambapo Serikali imeweza kuongeza hisa katika kitalu cha MnaziBay kutoka asilimia 20 hadi kufikia asilimia 40.

Ameeleza kuwa, Sekta ya gesi asilia ni muhimu kutokana na kuchagiza matumizi ya sekta nyingine ikiwemo matumizi ya gesi iliyoshindiliwa katika magari na kuunganisha mtandao wa gesi majumbani, miradi ambayo inafanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Lindi.

Akielezea kuhusu mafuta amesema Serikali imekuwa na mafanikio katika kusimamia na kudhibiti bei kikomo za bidhaa za mafuta na kuongeza kuwa bei ya ndani ya bidhaa za mafuta imeendelea kuwa himilivu kutokana na Serikali kuweka ruzuku kwenye bidhaa hiyo.

Kuhusu mfumo wa pamoja wa  kuagiza mafuta amesema kuwa  umeendelea kuimarika.

Kuhusu Sekta ya  umeme, Kapinga amesema kuwa Sekta hiyo ni moyo wa uchumi katika Taifa na kutanabaisha kuwa, mwaka 2021 uwezo wa kuzalisha umeme ulikuwa takribani megawati 1,600 na  hivi sasa ni takribani megawati 4,000.

Ameeleza kuwa,  kuongezeka kwa megawati hizo kunatokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika miradi ya kuzalisha umeme ukiwemo mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere.

Kwa upande wa miradi ya usafirishaji umeme, Kapinga amesema njia za kusafirisha umeme zilikuwa kilometa takribani 6,000 mwaka 2021 na sasa hivi zipo kilometa takribani 8,000 na njia za usambazaji  zimetoka kilometa 144,000 hadi kilometa 200,000.

Akielezea miradi ya umeme Vijijini, Kapinga amesema kwa kipindi cha miaka minne Serikali imekamilisha upelekaji wa umeme katika Vijiji vyote na hivi sasa Serikali imejikita kupeleka umeme katika Vitongoji.

Post a Comment

0 Comments