Na mwandishi wetu
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kimejipanga kwa umakini mkubwa kuhakikisha kinakiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 6, 2025 na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama unaoendelea katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Shaibu amesema ACT Wazalendo imejifunza kutokana na uzoefu wa historia ya vyama vingi nchini, kuanzia miaka ya 1990 hadi sasa.
Amesema tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ACT Wazalendo imekuwa ikiweka mkazo mkubwa kwenye mipango ya kimkakati, ikitathmini mambo yaliyofanywa vyema na wapinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, sambamba na kufanyia kazi maeneo ya udhaifu ambayo yamekuwa kikwazo kwa upinzani kwa miaka mingi.
Ado amesema chama chake kipo tayari na kina “silaha za kutosha” kisiasa, kimaadili na kimkakati, kuhakikisha mabadiliko ya uongozi wa nchi yanapatikana kwa njia ya kidemokrasia.
Kwa upande wake Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu akizungumza katika Mkutano huo wamechagua kushiriki uchaguzi sio kwa sababu ya mapenzi bali kwa sababu ya dhamira.
"Ninataka niweke wazi mbele ya wajumbe wote. Hatukuchagua kushiriki uchaguzi kwa sababu ya mapenzi. Tumechagua kushiriki kwa sababu ya dhamira. Dhamira ya kulinda haki ya kuchagua. Dhamira ya kurejesha thamani ya kura ili wananchi wawe na uwezo wa kuamua nani awe Kiongozi wao.” amesema Semu na kuongeza,
“Tumejifunza kutokana na historia, kususia hakujawahi kuleta mabadiliko. Mapambano ya kweli ni ya wale wanaojitosa uwanjani. Na sisi, ACT Wazalendo, tumeingia vitani na tutatoka na ushindi! Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia ipasavyo uchumi, huduma za jamii, na masuala ya utawala bora,".
Semu ameongeza "Watanzania wengi wanaishi katika umaskini, ukosefu wa ajira na uhakika wa vipato, wakiwa hawana huduma bora za kijamii, wakiishi kwa hofu, wakizuiwa kupaza sauti na kupewa matumaini hewa ya kesho iliyo njema. Tumeendelea kuwa taifa la wachache kunufaika na walio wengi kuteseka,".
0 Comments