Madai ya Matumizi Mabaya ya Magari na Rushwa Zazusha Mzozo Kati ya Wagombea CCM Wilaya ya Lushoto

 





Na mwandishi wetu

Baadhi ya Watia nia na wajumbe wamesema kuwa baada ya kura za maoni, wagombea sita walioteuliwa walipewa maelekezo ya kuhudhuria kampeni zilizoandaliwa kwa mpangilio maalum.

Walieleza kuwa kila mgombea alitakiwa kufika makao makuu ya wilaya saa 12:30 asubuhi kila siku, ambako magari ya kampeni yalitoka pamoja na jioni wote kurudishwa eneo hilo kwa ajili ya kurejea nyumbani.

Hata hivyo, walidai kuwa baadhi ya wagombea walikaidi agizo hilo kwa kutumia magari binafsi kufanya kampeni kinyume na utaratibu.

Walisema kuwa baadhi yao walikuwa wakitoa rushwa kupitia watu wao wa karibu, huku wakielekeza waziwazi wagombea wanaopaswa kuungwa mkono.

“Tulielekezwa tusitumie magari binafsi, lakini baadhi yao walitumia magari yao kuendesha kampeni za chinichini na kuwapa zawadi wapiga kura kupitia ndugu zao,” walisema mmoja wa wajumbe hao.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Lushoto, Nuru Mtoto amekiri kuwa na taarifa hizo, hata hivyo ametaka Mkuu wa Wilaya hiyo ndiyo atafutwe kwani ndiye mwenye vyombo vya ulinzi.

“Hili ni suala la Mkuu wa Wilaya kwa sababu ndiyo mwenye vyombo, mimi siwezi kuthibitisha. Hili suala niliambiwa lakini nimeliachia kwa sababu kuna vyombo. Wewe ukiongea na DC, yeye atakwambia kama kweli ilikuwa hivyo, yeye ndiyo anaweza kuthibitisha,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Zephania Sumaye alisisitiza kuwa CCM ni chama kinachozingatia kanuni na taratibu, na ndio maana wagombea wote walielekezwa kutumia usafiri wa pamoja ili kuondoa mazingira ya upendeleo au matumizi mabaya ya rasilimali.

Kuhusu madai ya rushwa, Sumaye alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa makini kuhakikisha hakuna mianya ya rushwa katika mchakato huo.
Alifafanua kuwa kesi chache zimeibuliwa dhidi ya watu wanaosadikiwa kutumwa na wagombea, ingawa bado uchunguzi unaendelea kubaini ukweli wa madai hayo.

“Wapo wanaodai wametumwa na wagombea lakini si kweli. Tukibaini ukweli kupitia uchunguzi, tutatoa taarifa rasmi,” aliongeza Sumaye.

Post a Comment

0 Comments