MARIAM MWINYI:VIJANA NI NGUVU YA SASA YA MAENDELEO

 



Na mwandishi wetu

Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa vijana ni nguvu ya sasa ya maendeleo ya Zanzibar, na si watu wa kuchukuliwa kama ahadi ya kesho.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Agosti 2025, alipofungua Jukwaa la East Africa Youth Business and Investment Expo 2025 lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Mkoa wa Kusini Unguja.

Amewahakikishia vijana kuwa Zanzibar iko tayari kuwa kitovu cha ubunifu na uwekezaji wa vijana katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, ameshauri vijana kutumia fursa zilizopo kwa kujipanga, kuwa na nidhamu, kuendelea kujifunza, na kushirikiana kutumia majukwaa mbalimbali kwa hatua za kimaendeleo.

Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa Taasisi ya ZMBF imefanikiwa kuwawezesha jumla ya vijana 602 kupitia programu za uwezeshaji wa kijamii na kiuchumi katika sekta ya mwani, ikiwemo kuwapatia boti zenye injini, mafunzo, ujenzi wa miundombinu ya kukaushia mwani, uhamasishaji wa vikundi vya kuweka na kukopa, pamoja na masoko ya kidijitali ya zao hilo.

Kwa upande mwingine, Mama Mariam Mwinyi amefafanua kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kwa kuibua mawazo bunifu, kuwapatia mitaji na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaojengwa kwa misingi ya maendeleo jumuishi na endelevu.













Post a Comment

0 Comments