Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu,kuelewa kuwa siku zote mambo ya ngoswe huachiwa ngoswe wenyewe kwani yanayoendelea ndani ya CCM yanawahusu wana CCM wenyewe.
Pia chama hicho kimemueleza Jussa atautambua ukweli wa mambo na kukubalika kwa Rais Dk Hussein Ali Mwinyi ifikapo Oktoba Mwaka huu.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis aliyesema matokeo ya Uchaguzi Mkuu ndio yatakayokata ngebe na kidomodomo cha Jussa.
Mbeto alisema kwa miaka yote tokea mwaka 1995 hadi 2020, CUF baadae ACT , vilikuwa vikimsimamisha mgombea mmoja wa urais Hayati Maalim Seif Sharif Hamad na CCM hakikuwahi kuhoji.
Alisema CCM hakikusema lolote au kuingilia matakwa ya demokrasia na maamuzi ya chama hicho wala kuhoji kwanini mgombea anakuwa mtu huyo huyo miaka kwa miaka.
"Ni ajabu kumsikia Ian Smithi wa Zanzibar akiingilia mambo ya CCM na kutaka Dk Mwinyi asiwe mgombea Urais Zanzibar . Tunaijua hofu alonayo Jussa na wenzake ni bidii,utayari na uchapakazi wa Rais Dk Mwinyi "Alisema Mbeto
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema kama kweli Jussa ni Mwanademokrasia wa kweli ilikuwaje miongo yote hiyo ndani chama chao wawe na mgombea mmoja wa kudumu .
"Jussa anza kutoa boriti kwenye jicho lako kabla hujakitoa kibanzi kwenye jicho la mwenzako. Maalim Seif amekuwa akigombea Urais kila mwaka hakuwahi kumkosoa .Mambo ya CCM hutawezi waachie waamue wana CCM wenyewe "Alisema Mbeto
Pia Katibu huyo Mwenezi amekitaka ACT kutoidanganye dunia kama mgombea wao wa Urais Zanzibar Othman Masoud Othman ana ubavu wa kumshinda Rais Dk Mwinyi.
Hata hivyo Mbeto aliendelea kumkanya Jussa huku akimtaka kuacha Siasa za jazba, uheke na udalali ,badala yake awe mtu muungwana kwani kuna maisha mengine baada ya uchaguzi na Siasa
"Huyu Ian Simiti wa Zanzibar hajui maana ya Siasa yeye muda wote anahemkwa na chuki, gere na wivu wa jikoni . Aachana na Siasa za Miaka ya 1950 wakati Zanzibar ikipigania uhuru .Siasa za ubaguzi na uhasama hazitakiwi tena Zanzibar na kizazi kipya" Alisiaitiza
Katibu huyo Mwenezi alimueleza kinaganaga Jussa kuwa ameshiriki kuwafanya mizengwe ili kuwazuia kina Juma Duni Haji na Mohamed Dedes wasigombea urais huku akimpigia debe Othman ili kulinda maslahi yake binafsi.
0 Comments