Na mwandishi wetu
Tume ya Tehama ikishirkiana na taasisi ya Korea Kusini (KISA) wamefungua mafunzo ya usalama wa mtandao leo Jumatatu Agosti 11, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama Dk Nkundwe Mwasaga amesema ili watu watumie fursa zitokanazo na uchumi wa kidijitali inabidi imani ya mifumo iwepo kwa watumiaji.
“Ni vizuri wataalamu wetu wajifunze kwa sababu sikuhizi watu wanaingilia mifumo na udukuzi,"amesema.
Amesema ujuzi wanaoupata watu hao 33 wataenda kuwapatia na wenzao wengine.
“tunahitaji kuwa na wataalamu wengi ili kuwa na uchumi wa kidijitali kuongeza wawekezaji, watu kuwa huru kutumia mitandao yenye fursa mbalimbali.
“Sasa hivi huduma nyingi zinafanyikia mtandaoni, maisha ya watu wengi wanategemea mifumo, malipo, huduma mbalimbali za kiserikali kwahiyo wataalamu wanahitajika kila wilaya, tarafa na sehemu zote bila kusahau elimu kwa wananchi,” amesema.
Kwa upande wake, Minyoung Kim amesema ni muhimu kwenda na nyakati ukirejea Mapinduzi ya AI yaliyopo duniani hivyo mafunzo kama hayo yanasaidia wataalamu wa Kitanzania huku akiahidi kuendeleza ushirikiano.
Venance Mwanjabike kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kitengo cha Tehama amesema matukio ya AI, ikiwemo teknolojia za Deepfake zinahitaji uchunguzi wa kitaalamu.
“Jinsi ya kujua video hii imetengenezwa ama haijatengenezwa ni changamoto inayohitaji ujuzi wa kitaalamu pamoja na vifaa ikiwemo software. Tunahitaji kuongeza wataalamu pamoja na mafunzo kama haya,” amesema.
0 Comments