■Mpango ni kuwa ifikapo mwaka 2030 Sekta ya Kilimo kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa.
■Rais , Dkt.Samia Suluhu Hassan azindua Maabara ya kisasa ya kilimo jijini Dodoma.
■Serikali imeongeza bajeti ya utafiti wa kilimo hadi kufikia asilimia tano.
*Dodoma*
Katika kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 10 katika Pato la Taifa , tayari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeandaa miongozo ya kilimo cha jiolojia na kilimo mseto.
Hayo, yamebainishwa leo Agosti 8, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihairisha maonesho ya kimataifa ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Dkt. Samia amesema kuwa, katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Awamu ya tatu tayari Serikali kupitia mamlaka husika imeandaa miongozo mbalimbali itakayowezesha kilimo cha Jiolojia na Kilimo Mseto.
Akielezea kuhusu maabara ya kisasa ya utafiti wa mbegu , udongo na mimea , Dkt.Samia ameeleza kuwa, Serikali imeongeza bajeti ya utafiti wa kilimo hadi kufikia asilimia tano ambapo kupitia maabara ya kisasa wataalam wa masuala ya kilimo na udongo watapata fursa ya kufanya tafiti za mbegu bora zenye kustahimili hali ya hewa na kemikali za udongo kabla ya kusambazwa kwa wakulima.
*Kilimo cha jiolojia ni nini?*
Kilimo cha Jiolojia ni dhana mpya inayochanganya maarifa ya jiolojia (elimu ya miamba, madini, udongo, na historia ya dunia) na kilimo ili kuboresha tija na uendelevu wa uzalishaji wa kilimo.
Hii inahusisha kutumia taarifa za kijiolojia kuelewa sifa za udongo, upatikanaji wa virutubisho, na hali ya maji chini ya ardhi ili kusaidia wakulima kuchagua mazao sahihi na mbinu bora za kilimo.
Miongozo ya Kilimo cha Jiolojia ni pamoja na uchambuzi wa udongo kwa Mtazamo wa Jiolojia, kuchunguza aina ya miamba inayounda udongo katika eneo husika, kutambua madini yaliyomo kwenye udongo mfano fosforasi , potasiamu na kalsiamu , uelewa wa sifa za udongo kama vile asidi (pH), hususani kwenye uwezo wa kushikilia maji , na rutuba , kutumia ramani za jiolojia zenye kuonyesha maeneo yenye udongo bora kwa mazao fulani.
Kilimo cha jiolojia kinasaidia kuchimba visima kwa ufanisi na kupunguza gharama, kutumia madini ya asili kama mbolea kwa mfano katika miamba ya phosphate na chokaa.
Kupunguza utegemezi wa mbolea za viwandani kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya nchi.
Faida za Kilimo cha Jiolojia ni pamoja na kuongeza uzalishaji kwa kuchagua mazao sahihi kulingana na aina ya udongo.
*# Vision 2030: MadiniNiMaishaNaUtajiri*
0 Comments