Na mwandishi wetu
Amshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kutoa Milioni 900 kuboresha miundombinu Hospitali ya Wilaya ya Meru
Arusha, Tanzania – Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mapinduzi makubwa yaliyofanywa kwenye sekta ya afya mkoani Arusha. Hospitali ya Wilaya ya Meru, iliyoko Wilayani Arumeru, imepokea shilingi Milioni 900 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya huduma za afya.
CPA Makalla ameyasema hayo Jumanne, Septemba 09, 2025, wakati akitembelea na kukagua hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma katika majengo mapya manne ya hospitali hiyo:
Jengo la Wagonjwa wa Nje
Jengo la Maabara
Jengo la Bohari ya Dawa
Jengo la Kuchomea Taka na Wagonjwa wa Dharura
Majengo haya tayari yameanza kutoa huduma kwa wagonjwa, na yamepunguza muda wa kuhudumiwa kutoka saa nane hadi saa mbili, hatua inayoongeza ufanisi katika utoaji huduma.
"Faida za uwekezaji huu mkubwa ni pamoja na kupunguza masaa ya kuwahudumia wagonjwa, uwepo wa vipimo 38 ambavyo vimepunguza rufaa za wagonjwa kwenda kwenye hospitali za rufaa kama vile KCMC na Mount Meru. Haya ni mafanikio makubwa kwa serikali yetu. Niwaombe watoa huduma wote kutumia maboresho haya kutoa huduma bora, kuanzia mapokezi, lugha nzuri, hadi matibabu," amesema CPA Makalla.
Aidha, CPA Makalla amesisitiza kuwa maboresho haya yameambatana na ongezeko la bajeti kwa ajili ya ununua dawa na vifaa tiba, pamoja na ukarabati wa jengo la watoto wachanga na watoto njiti wenye mahitaji maalumu ya uangalizi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Meru, Dkt. Elisante Fabian, ameeleza kuwa maboresho haya yameongeza wigo wa huduma na idadi ya wagonjwa, mapato ya hospitali, na uwezo wa hospitali kufanya vipimo vyote 38 vinavyohitajika katika hospitali za wilaya nchini.
0 Comments