DOYO AGUSIA MKONGE KAMA URITHI WA TANGANYIKA, AHIDI KUREJESHA THAMANI YAKE

 



Na Mwandishi Wetu

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiwa Korogwe amezungumzia zao la mkonge na kulihusisha na historia ya taifa tangu enzi za ukoloni, ambapo Tanga ilijulikana kimataifa kama kitovu cha uzalishaji wa nyuzi za mkonge.

Hata hivyo, amesema kwa miongo mingi wakulima wa mkonge wamekumbwa na changamoto za soko, teknolojia duni na ukosefu wa viwanda vya kuchakata kwa kiwango cha kisasa, hali iliyowalazimu kuishi kwa matumaini badala ya kunufaika na jasho lao.

Katika kampeni zake wilayani Korogwe, Mhe. Doyo aliibua upya mjadala kuhusu thamani ya zao hilo, akiahidi kujenga kiwanda cha kisasa cha kuchakata mkonge na kuhakikisha wakulima wanapatiwa pembejeo bure.

“Mkonge unaweza kututoa kwenye umasikini. Tatizo limekuwa ni teknolojia ya kizamani na ukosefu wa dhamira ya kisiasa. Nikipata ridhaa ya kuwa Rais, nitahakikisha tunaongeza thamani ya zao hili kwa manufaa ya wananchi,” alisema Doyo.

Wataalamu wa kilimo wanasema mkonge una nafasi kubwa katika viwanda vya nguo, nyuzi, kamba na bidhaa nyinginezo zinazohitajika kimataifa. Wakati mataifa ya Amerika Kusini na Asia yamewekeza katika teknolojia za kisasa, Tanzania bado imeendelea kutumia mbinu za kizamani zinazopunguza ubora wa zao hilo.

Aidha, Doyo alisema iwapo wananchi wa Korogwe na maeneo mengine watamchagua, atahakikisha kiwanda kipya kitawanufaisha wakulima kwa kuwawezesha kuuza bidhaa zilizo ongezwa thamani badala ya malighafi ghafi pekee. Hatua hiyo, alisema, itaongeza kipato cha wakulima na kuchochea ajira mpya kwa vijana na wanawake nchini.

Kwa miaka mingi, wakulima wa Korogwe wamelalamikia mikopo yenye masharti magumu na pembejeo zisizo na ubora. Nikipata nafasi, nitafuta mikopo yenye riba kubwa na kusisitiza utoaji wa fedha za asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri kwa riba nafuu,” aliongeza Doyo.

Ahadi hizo zimepokelewa kwa shangwe na wananchi wa Korogwe, hususan wanawake ambao mara nyingi wamekuwa wahanga wa mikopo kandamizi.

Kampeni za NLD zinaendelea, huku msafara wa mgombea huyo wa urais ukielekea Lushoto, Handeni, Kilindi na hatimaye Kiteto






Post a Comment

0 Comments