Na Mwandishi Wetu, Arusha
Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inaendelea kujidhihirisha kama lulu mpya ya utalii nchini, hususani katika ukanda wa kaskazini, ikiwavutia wageni wa ndani na nje ya nchi kwa mandhari yake ya kipekee na utajiri wa spishi mbalimbali za wanyamapori.
Leo, Septemba 8, 2025, hifadhi hiyo imepokea tena kundi la wageni wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali kupitia kampuni maarufu ya utalii, Ranger Safaris & Tours, yenye makao yake jijini Arusha.
Zaidi ya wageni 20 kutoka Denmark, Australia na New Zealand wametembelea hifadhi hiyo na kueleza kufurahishwa kwao na mandhari ya kuvutia, urithi wa kiasili na vivutio adimu vinavyopatikana hifadhini humo.
Aidha, wageni hao wameeleza kuridhishwa na ubora wa huduma ndani ya Makuyuni Wildlife Park, huku baadhi yao wakiahidi kurejea tena mwezi Novemba mwaka huu kwa ziara ya pili.
Wakizungumza baada ya kutembelea hifadhi na kujionea vivutio, wageni hao pia wameahidi kuendelea kuitangaza Makuyuni Wildlife Park katika masoko ya kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza umaarufu na kuhamasisha wageni wengi zaidi kuitembelea.
Kwa sasa, Makuyuni Wildlife Park iliyopo mkoani Arusha, inajitokeza kama moja ya hifadhi mpya zenye fursa kubwa za kukuza sekta ya utalii nchini, ikionekana kukua kwa kasi katika viwango vya ubora na uwezo wa kuwaridhisha wageni wa hadhi ya juu.
0 Comments