Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya Jamii Mpya Tanzania imetangaza mpango kabambe wa kitaifa wa kuhamasisha wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ikiwalenga zaidi vijana na wanawake, huku ikipinga miito ya kisiasa inayohamasisha wananchi wasusie uchaguzi huo.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Kitaifa wa taasisi hiyo, Ally Makwiro, alisema Jamii Mpya imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza mshikamano wa kijamii kupitia kampeni mbalimbali zikiwemo uhamasishaji wa chanjo ya corona, utalii wa ndani, sensa ya watu na makazi, pamoja na uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Makwiro alionya dhidi ya makundi na wanasiasa wanaotaka wananchi wasishiriki uchaguzi huo, akisema kitendo hicho ni hatari kwa mshikamano wa taifa na si kwa masilahi ya wananchi bali ni tamaa ya madaraka.
“Chuki binafsi za baadhi ya viongozi haziwezi kuwa sababu ya kuwapotosha wananchi na kuhatarisha amani ya nchi. Ni wajibu wa kila Mtanzania kuwapuuza na kuwakemea,” alisema Makwiro.
Ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga zaidi vijana, ambao mara nyingi hutumiwa katika machafuko ya kisiasa, pamoja na wanawake wanaobeba mzigo wa maisha magumu wakati wa vurugu. Jamii Mpya itatumia njia mbalimbali za kuelimisha wananchi, ikiwemo makongamano, warsha, semina, matembezi ya amani, mitandao ya kijamii na vipeperushi, kwa lengo la kuwafikia Watanzania zaidi ya milioni 10.
Kwa upande wake, Sambe Wayanga, mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo, amesisitiza umuhimu wa vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
"Jamii Mpya ni jamii chanya inayolinda amani ya Tanzania. Vijana na wanawake wanapaswa kuelimishwa ili wachague viongozi wenye dira na kuepuka matendo yanayohatarisha mshikamano wa taifa,” alisema Wayanga.
Wayanga pia aliwataka wasichana waliokomaa kiumri kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia, ili wapate nafasi ya sauti na utetezi wao kusikika.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, mikakati ya uhamasishaji inatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya vijana na wanawake kushiriki Katika uchagunzi mkuu oktoba 29,2025
0 Comments