Doyo, NLD: Tukichaguliwa, Tutageuza Kilindi Kitovu cha Biashara

 




Kilindi, Tanga — Septemba 2025

Mgombea Urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiwa safarini kuelekea Kiteto mkoani Manyara, aliendelea na kampeni zake kwa kuhutubia wananchi wa Kijiji cha Kwediboma, Wilaya ya Kilindi, ambapo alieleza sera na mipango yake ya maendeleo endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na wakazi wa Kwediboma, Mhe. Doyo alisema kuwa wananchi wa Kilindi wamesahaulika kimaendeleo kwa muda mrefu, hususan katika sekta za barabara, huduma ya maji safi na afya. Aliongeza kuwa Kilindi haina barabara inayopitika kwa mwaka mzima ndani ya miaka 64 ya uhuru wa Tanzania, jambo linalokwamisha wananchi kusafirisha mazao yao kwa wakati.

> “Msingi wa maendeleo ni barabara. Wingi wa mazao mnayolima, ikiwemo mahindi na maharage, thamani yake inapotea kwa madalali kutokana na ukosefu wa barabara bora. Tukishapewa fursa ya kuongoza, tutajenga barabara hizi kwa kiwango cha zege kinachokidhi hali ya kijiografia ya mabonde ya eneo hili, hususan barabara ya Kilindi–Handeni,” alisema Mhe. Doyo.

Aidha, Mhe. Doyo alibainisha kuwa amekutana na nyumba zilizobomolewa ili kupisha mradi wa ujenzi wa barabara ulioanzishwa enzi za utawala wa Hayati Rais John Magufuli, miaka minne iliyopita, lakini wananchi bado hawajalipwa fidia. Ameahidi kulipa fidia kwa wote walioguswa na bomoa bomoa hiyo ili kufanikisha mradi huo.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Pogora Ibrahim Pogora, alisema kuwa Doyo ni kiongozi mzalendo anayezingatia haki na usawa. Aliongeza kuwa wananchi wa Kilindi wanapaswa kuzingatia changamoto zinazowakabili kila siku na kumpigia kura Mhe. Doyo ili kuona thamani ya kura zao.

Mwenyekiti wa Kigoda cha Kina Mama Taifa wa Chama cha NLD, Bi. Saidati Fundi, alisema Tanzania inahitaji mabadiliko ya kweli yatakayopatikana kupitia NLD:

> “Nchi haiwezi kupiga hatua ikiwa hatutakuwa na dhamira ya kumaliza matatizo yanayotokana na sera mbovu. Wananchi chagueni viongozi wa NLD, Mhe. Doyo ana dhamira ya kweli.”

Naye Muhamasishaji Mkuu wa Kampeni kwa upande wa kina mama, Adija Dikulumbali, aliwahimiza wanawake kutafakari changamoto zinazowakabili, hususan gharama za huduma za afya kwa wajawazito.

> “Thamani ya kura yenu ipo pale ambapo mtachagua kiongozi atakayewaletee maendeleo halisi. Mmesahaulika kwa muda mrefu, sasa ni wakati wa kuibuka kidedea kwa thamani ya kura yenu,” alisema.

Msafara wa kampeni wa Mhe. Doyo umeelekea Kiteto, Manyara, ambapo kampeni za kumnadi zinaendelea huku Chama cha NLD kikijivunia sera zake zinazosisitiza usawa, uzalendo, haki na maendeleo ya wananchi wa Tanzania.



Post a Comment

0 Comments