MHANDISI MRAMBA NA JICA WAJADILI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA NISHATI

 



📌 Ni wa usafirishaji umeme kutoka Tanzania hadi Uganda na Dodoma Ring Circuit
📌 Awasisitiza JICA kuwajengea uwezo wataalam wazawa katika usanifu wa mitandao ya usambazaji Gesi Asilia

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amekutana na wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa ajili ya kujadili hali ya utekelezaji wa miradi ya Nishati inayofadhiliwa na shirika hilo, kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi.

Kikao hicho kimefanyika Septemba 8, 2025, katika ofisi za Wizara ya Nishati Mtumba, jijini Dodoma, ambapo pande hizo mbili pia zimejadili suala la kujengea uwezo wataalam wa Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), hususan katika usanifu wa mitandao ya usambazaji wa gesi asilia.

Miradi iliyojadiliwa kwa kina katika kikao hicho ni mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tanzania hadi Uganda (UTIP) na mradi wa Dodoma Ring Circuit, ambao unalenga kuongeza uimara wa upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dodoma.

Katika kikao hicho, Mhandisi Mramba alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa mradi wa mfano wa usambazaji gesi asilia katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ambao utakuwa kielelezo cha manufaa ya gesi asilia iliyogunduliwa nchini na kuchangia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, Mramba aliishukuru JICA kwa kuendelea kufadhili miradi ya nishati, akibainisha kuwa imekuwa chachu ya maendeleo hususan katika Jiji la Dodoma linalokua kwa kasi.










Post a Comment

0 Comments