📌 Awahimiza wananchi wa Namonge kujitokeza kupiga kura Oktoba 29
📌 Asema shilingi bilioni 200 kukopeshwa kwa vijana
Bukombe, Geita
Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka Biteko, amewaasa wananchi wa Kata ya Namonge kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais, akisisitiza kuwa kumchagua yeye ni kuchagua maendeleo ya kweli.
Dkt. Biteko alitoa wito huo Septemba 9, 2025 katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika wilayani Bukombe, mkoani Geita, ambapo alieleza namna serikali ya Rais Samia ilivyobadilisha sura ya maendeleo ya kata hiyo.
“Kata hii haikuwa na barabara ya kutoka Uyovu - Namonge - Nyalamandula, haikuwa na zahanati wala shule za kutosha, hivyo ilikuwa nyuma kimaendeleo. Lakini sasa maendeleo yameanza kushuhudiwa kwa vitendo,” alisema.
Alifafanua kuwa serikali imetekeleza miradi muhimu ya kijamii ikiwemo ujenzi wa zahanati, shule mpya na kituo cha afya, hatua zilizosaidia kuboresha maisha ya wananchi.
Ahadi za Maendeleo
Dkt. Biteko aliahidi iwapo atachaguliwa kuendelea kuongeza wodi na zahanati, kuboresha shule na kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma muhimu za kijamii.
“Tunataka watu wa Namonge waishi kama Watanzania wa daraja la juu. Tumekuja hapa kuomba kura ili tumchague Rais Samia kwa vile kumchagua yeye ni kuchagua maendeleo,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa CCM inalenga kuifanya Namonge kuwa kituo cha kilimo kupitia ujenzi wa barabara, hospitali na miradi ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Kwa mujibu wa Biteko, serikali pia imepanga kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya vijana, sambamba na mikopo ya wanawake na watu wenye ulemavu, ili kuwawezesha kiuchumi.
Ushirikiano wa Viongozi
Katika mkutano huo, alimnadi pia mgombea udiwani wa Namonge, Mlalu Bundala, akimtaja kama kiongozi makini anayejua changamoto za wananchi na atakayesimamia maendeleo ya kata hiyo.
Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita, Amani Msuwa, aliwahimiza wananchi kumpigia kura Rais Samia pamoja na Dkt. Biteko, akisisitiza kuwa miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia katika Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Bundala, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kueleza namna miradi ya maendeleo ilivyotekelezwa katika kata hiyo, ikiwemo barabara ya km 61, mtandao wa maji Namonge, shule za msingi na sekondari pamoja na kituo cha afya.
Aidha, alisema vijiji vyote katika kata hiyo vimeunganishwa na mtandao wa umeme huku jitihada za kufikisha huduma hiyo kwenye vitongoji zikiendelea.
0 Comments